MABAO aliyofunga juzi Ijumaa na mshambuliaji wa Tausi FC, Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ yamemfanya mkongwe huyo kuwa na rekodi tamu ya mchezaji aliyeifunga Yanga Princess mabao mengi zaidi akifikisha 16 kwa sasa kupitia timu tofauti.
Tausi FC iliyopanda Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu huu ilianza ligi kwa kupokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Yanga Princess katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Mwenge Dar es Salaam, huku mabao mawili ya kufutia machozi ya wageni bao wa WPL yakiwekwa kimiani na Gaucho.
Gaucho aliyewahi kutamba na Mlandizi Queens na Simba Queens pia ndiye mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kipekee ya kufunga hat-trick tatu katika mechi ya Dabi ya Kariakoo kabla ya kuhamishia makali yake Tausi alikokuwa pia mwiba mkali kwa wananchi hao wanapokutana.
Mbali na hat-trick hizo, pia Gaucho katika mechi mbili nyingine alifunga mabao manne na sasa akiwa na Tausi amefunga mabao mawili akifikisha jumla 16.
Akiwa Simba aliisaidia kuipa ubingwa ya Ligi ya Wanawake mara nne na kuifanya kuwa moja ya timu zilizokuwa na ushindani mkubwa hasa eneo la ushambuliaji.
Ubora wake haukuishia tu kwa Simba kwani nyota huyo wa zamani wa Mlandizi Queens na Shabab Atlas ya Morocco alikuwa na msaada kwa timu ya taifa, Twiga Stars.
Akizungumzia kuhusu kuwafunga Yanga Princess kila anapokutana nao Gaucho amesema; “Sio Yanga tu, mimi napenda sana ushindani, kuna chipukizi wengi, hivyo napambana kila siku ili kuonyesha nilichonacho na sio kwamba nawakamia Yanga.”