TUME ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeanza kuhoji majeruhi na baadhi ya ndugu waliopoteza wapendwa wao kwenye vurugu hizo, huku majeruhi hao wakishauri vijana kujiepusha na vurugu zinazoweza kusababisha amani kutoweka nchini.

Mahojiano hayo yalifanyika mkoani Dar es Salaam jana ambapo tume hiyo ilifanya kikao cha wazi na wananchi kukusanya mapendekezo ya baadhi ya waathirika wa vurugu hizo.

Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Othman Chande alisema tume hiyo imeanza kukusanya maoni kwa wananchi ili kupata mapendekezo ya kutafuta suluhisho kutoka kwa wadau.

“Tunawashukuru kwa ujasiri wa kuja mbele ya tume na kutueleza yaliyotokea kwa uwazi. Sisi tumetumwa kupata ushahidi wa yaliyotokea tuweze kupendekeza… Tunawapa pole na tunaomba Mungu atusimamie kama taifa,” alisema.

Katika kikao hicho, tume hiyo ilihoji juu ya mazingira, maeneo na muda wa matukio ya baadhi ya majeruhi walivyojeruhiwa.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue aliiwaambia majeruhi hao ushahidi walioutoa ni njia ya kutibu taifa kutokana na mambo yaliyotokea.

Aliwataka wananchi hao kueleza yaliyotokea kwa uwazi ili tume ishauri kwa usahihi.

Kadhalika, tume imetoa pole kwa majeruhi wote na waliopoteza wapendwa wao katika vurugu hizo, wakisisitiza kuwa sio tukio la kawaida na halijazoeleka kwa wananchi wa Tanzania.

“Tunawapa pole. Tunajua mna machungu lakini tunawaombea kwa Mungu awapunguzie machungu yenu na awajaalie amani siku zijazo,” ilisema tume hiyo.

Wakitoa mapendekezo yao mbele ya tume hiyo, baadhi ya waathirika walishauri serikali kuendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi kupitia vyombo vyao vya usalama, kwa sababu haijawahi kutokea vurugu kama zilizotokea siku ya uchaguzi nchini.

Walishauri pia vijana kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu sambamba na kufuata sheria zinazowekwa na viongozi wa nchi.

“Tunamuomba Mungu miaka mingine isitokee tena kama yaliyotokea kwenye uchaguzi huu… kiukweli serikali ijitahidi sisi vijana tuwe na usalama kwa sababu hatujazoea kuona machafuko katika nchi yetu na haijawahi kutokea,” alisema mmoja wa waathirika hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *