Waumini wakumbushwa kuishi kwa imaniWaumini wakumbushwa kuishi kwa imani

DODOMA; WAUMINI nchini wamekumbushwa kuishi maisha ya imani ili kuandika historia nzuri wakiwa duniani na hata wakitangulia mbele ya haki kama alivyofanya Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, mwaka huu.

Hayo yalisemwa jana na Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Padri Emmanuel Mtambo wakati wa misa ya kumuaga Jenista anayetarajiwa kuzikwa Desemba 16, mwaka huu katika Kijiji cha Ruanda, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

“Niwaombe waamini wote muandike mahubiri yenu ili siku ya kuondoka tusiandike mahubiri yetu. Kwa mfano, mkiishi maisha ya imani kama Jenista kwa kununua vitambaa, kusaidia jamii na kuiishi imani vizuri, mahubiri yetu hayatakuwa tofauti na hakutakuwa na matatizo baada ya mahubiri zaidi utakumbukwa kwa kuacha alama,” alisema.

Alisema kanisa litamkumbuka Jenista kwa unyenyekevu, ushirikiano, kujitolea, aliyempenda Kristo, mwenye mapenzi ya kweli kwa jamii na mshiriki mzuri katika kusali bila kuwa na ulinzi.

Aliongeza kuwa kanisa litamkumbuka kwa mahudhurio yake ya misa za asubuhi iwe mvua imenyesha au haijanyesha, kwa kupenda kufanya matendo ya huruma kwa kusaidia watu wenye uhitaji.

“Alikuwa na unyenyekevu wa aina yake. Katika misa alikuwa na nia zake kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 31, kila mwaka ikiwemo kuwaombea Rais, Makamu wa Rais na viongozi wengine wote na familia yake kwa ujumla. Alitoa nguo na vitu mbalimbali kusaidia masikini na hakutaka sadaka hizo zitangazwe, bali alikuwa akijisikia humtuma dereva wake alete kanisani,” alisema.

Padri Mtambo alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa parokia, akieleza kuwa amehuzunika kumpoteza muumini wa aina hiyo huku akibainisha kuwa hakutarajia kifo hicho kwa kuwa alifahamu tatizo la afya alilokuwa nalo halikuwa kubwa wala hatarishi kwa maisha yake.

Kwa upande wake Padri kutoka Parokia ya Peramiho ambaye kwa sasa anahudumu Parokia ya Nkuhungu, Dk Exavery Komba alisema Jenista alikuwa mlezi wake tangu mwaka 1999 hadi sasa; ni dhahiri hakuna mwanadamu anayemdai wala Mungu, kwa kuwa aliyotumwa kuyafanya ameyafanya.

“Alikuwa mlezi wangu na mshauri. Alipenda watu wote bila kujali elimu, dini, umri wala kabila. Zaidi, ya yote aliipenda serikali na kila ukiongea naye alizungumzia suala la kutunza amani. Kikubwa tunamuachia Mungu, lakini tukumbuke ametuachia kitabu cha kujifunza katika imani, uhusiano na hata katika siasa,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *