CEASIAA Queens imetaja sababu ya nyota wake wawili wa kigeni, Anita Adongo na Diana Cherono kutoonekana uwanjani huku changamoto ya vibali ikiwa mojawapo.

Timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya sita msimu uliopita kwenye mechi 18, ilishinda sita, sare tatu na kupoteza mechi tisa, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 37, ikikusanya pointi 21.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema mshambuliaji Cherono aliyejiunga msimu huu akitokea Vihiga Queens ya Kenya na Adongo aliyekuwapo tangu msimu uliopita wanashughulikiwa vibali vyao.

Chobanka amesema, timu hiyo inaendelea kufanya mchakato wa kupata vibali ili waweze kucheza na kuisaidia timu hiyo.

“Nafikiri labda watakosa mechi mbili lakini wanaweza kuiwahi mechi na Simba, ni wachezaji muhimu kwa timu na natamani mambo yakae sawa mapema ili waweze kuisaidia timu,” amesema na kuongeza:

“Vibali vya wachezaji imekuwa changamoto kubwa kwa hizi timu za madaraja ya kati, timu kubwa zinapata ahueni wakipitia mgongo wa timu kubwa hivyo huku chini ni ngumu kupata vibali vya wachezaji wote wa kigeni kwa wakati mmoja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *