Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameimwagia sifa Tanzania, akiielezea kuwa ni kielelezo cha amani barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Kulingana na Mtendaji Mkuu huyo wa UN, Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani, akisisitiza kuwa dunia nzima, inalitazama taifa hilo kama mfano wa kuigwa.
Hata hivyo, Guterres, ambaye alikuwa akizungumza baada ya kupokea Ujumbe Maalumu kutoka Tanzania, Disemba 14, 2025, alisema kuwa sifa hiyo nzuri ya Tanzania, ilipitia majaribio wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, licha ya kufanikiwa kuyavuka.
Aidha, Guterres alisema kuwa anafurahishwa kuona Tanzania ikiendelea kuwa na umoja, licha ya changamoto hizo, akisisitizia umuhimu wa kuwa na mazungumzo ya kitaifa kutafuta suluhu ya vurugu baada ya Uchaguzi Mkuu.
Kulingana na Guterres, Umoja wa Mataifa upo tayari kutoa msaada kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya uvunjifu wa Amani, maarufu kama Tume ya Jaji Othman Chande.
