Kufuatia shambulizi hilo, Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese aliitisha mkutano wa viongozi wa majimbo na wilaya, na kwa pamoja wakakubaliana kuimarisha sheria za bunduki kote nchini humo.
Ofisi ya Albanese imesema wamekubaliana kuangalia njia za kuboresha ukaguzi wa wamiliki wa silaha, kuzuia watu wasio raia kupata leseni za bunduki na kupunguza aina za silaha ambazo ni halali.
Australia yatiliwa shaka nia yao ya kukabiliana na chuki dhidi ya wayahudi
Huku Australia ikiwa imelaani shambulio hilo, watu wengi katika jamii ya Wayahudi wametilia shaka azma yake ya kupambana na chuki dhidi yao.
Hii leo, mjumbe maalum wa Australia wa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi, Jillian Segal, amesema chuki hiyo imekuwa ikipenya kwa miaka mingi katika jamii lakini hawajajitokeza kwa nguvu kukabiliana nayo.
Segal ameliambia shirika la habari la ABC kwamba shambulizi la Bondi ni shambulizi dhidi ya Australia na sio tu kwa jamii ya Wayahudi.
Kwa upande wake, mkuu wa jamii ya Wayahudi ya Australia Robert Gregory ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ufyatuaji risasi wa Bondi ulikuwa “janga lakini ambalo lilikuwa wazi kabisa”.
Ameongeza kusema serikali imeshindwa kuchukuwa hatua za kutosha kuilinda jamii hiyo.
Netanyahu alaani shambulizi dhidi ya Wayahudi nchini Australia
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye ameikosoa Australia kwa kuziponda sera za vita za nchi yake, ameishtumu serikali ya nchi hiyo kwa “kumwaga mafuta kwenye moto wa chuki dhidi ya Wayahudi” kwa kutochukua hatua katika miezi ya kueleka shambulizi hilo.
Hapo jana baba na mwanawe walifyatua risasi dhidi ya umati wa watu katika ufukwe huo wa Bondi kwa ajili ya kuanza kwa sherehe za Hanukkah .
Msichana mwenye umri wa miaka 10, manusura wa mauaji ya kimbari na kiongozi mmoja wa kidini walikuwa miongoni mwa waliouawa, huku watu wengine 42 wakipelekwa hospitalini wakiwa na majeraha ya risasi pamoja na majeraha mengine.
Ahmed al Ahmed, mkazi mmoja wa Sydney aliyepambana na mshambuliaji mmoja na kumpokonya bunduki, anaendelea kupata nafuu hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na majeraha ya risasi kwenye mkono wake. Haya ni kwa mujibu wa familia yake.