Tangazo hilo lilitolewa wakati marais wa kanda hiyo walipokusanyika nchini Nigeria kwa mkutano wa kila mwaka. Ajenda ya mkutano huo ilitawaliwa na mapinduzi hivi karibuni ya Guinea-Bissau na jaribio la mapinduzi lililozimwa nchini Benin.
Baada ya mkutano huo wa kilele uliofanyika mjini Abuja kukamilika jana jioni, rais wa halmshauri kuu ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, Omar Alieu Touray, aliwaambia waandishi habari kwamba, wataweka vikwazo maalum kwa watu au mashirika yatakayokuwa visiki dhidi ya mchakato wa mpito
Touray aliongeza kuwa kikosi cha ECOWAS cha kulinda amani kilichopelekwa Guinea-Bissau, kiliidhinishwa ili kuwalinda viongozi wote wa kisiasa na taasisi za kitaifa katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi lakini ambalo limezongwa na mapinduzi tangu 2022.
Julius Maada Bio: mpangilio wa kidemokrasia unajaribiwa
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS, alisema waasisi wa jumuiya hiyo walielewa fika kwamba demokrasia haiwezi kutenganishwa na amani, haki na maendeleo na kwamba mapinduzi Guinea-Bissau na jaribio kama hilo nchini Benin ni ukumbusho kwamba demokrasia inahitaji uangalizi wa kudumu na hatua za kimaadili.
“Leo, mpangilio wa kidemokrasia unajaribiwa. Kurejea kwa mabadiliko ambayo ni kinyume na katiba kunatishia uthabiti wa kanda yetu, kunadhoofisha haki za raia wetu, na kunapunguza mustakabali wetu wa pamoja,” amesema Bio.
Mapinduzi hayo ya kijeshi ya Guinea-Bissau na vilevile jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa nchini Benin wiki moja iliyopita, yameitikisa jumuiya ya ECOWAS, na iliyalaani vikali wakati wa mkutano wake wa kilele siku ya Jumapili.
Touray: Wanajeshi zaidi kulinda amani Guinea-Bissau
Jaribio la mapinduzi lililoshindikana nchini Benin lilisababisha Nigeria kutuma ndege za kivita na wanajeshi, pamoja na askari kutoka Ivory Coast, ili kuimarisha serikali ya kiraia. ECOWAS imesema wanajeshi zaidi wako njiani kutoka Ghana na Sierra Leone.
Jumuiya ya ECOWAS imekumbwa na misururu ya mapinduzi ya kijeshi kati ya mwaka 2020 na 2023 ikiwemo nchini Burkina Faso, Guinea, Mali na Niger. Nchi hizo zote zikiwa bado katika utawala wa kijeshi hadi sasa.
Kikao cha kilele cha Jumapili kilifanyika katika ukumbi wa mikutano ulioko kwenye eneo tulivu na lenye ulinzi mkali karibu na ikulu ya Aso Rock.
Kikao hicho kilipangwa kabla ya matukio ya mapinduzi mawili ya hivi karibuni, lakini yote yamekuwa ajenda kuu, sambamba na uchaguzi wa Desemba 28 nchini Guinea.
Usalama wa Sahel
Kiongozi wa utawala wa kijeshi, Mamady Doumbouya, aliwania urais licha ya ahadi ya awali ya kutofanya hivyo, huku kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni na waziri mkuu wa zamani, Cellou Dalein Diallo, akiondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Hata hivyo, Touray alisifia uchaguzi wa Guinea kama hatua muhimu kwenye mchakato wa mpito.
Mkutano huo wa kilelle pia ulijadili usalama wa kanda ya Sahel ambako makundi ya wanamgambo wa kidini yanaendeleza machafuko Burkina Faso, Mali na Niger.
Nchi hizo ziliunda muungano wao wenyewe wa nchi za Sahel (AES). Touray amekuwa akitoa wito kwa ECOWAS kufanya mazungumzo na muungano wa nchi hizo tatu.
(AFPE)
