Akitoa agizo la kutofanyika maandamano katika eneo zima la mji wa kinshasa, gavana Daniel Bumba amesema kuwa hayo yanatokana na sababu za kiusalama haswa wakati huu taifa likiwa kwenye hatari.
“Hakuna maandamano yatakayoruhusiwa ikiwa yataweza kuvuruga usalama wa umma. Nawaomba wananchi wabaki makini na wenye tahadhari. Njia bora ya kuonesha mshikamano wetu na wananchi wa Mashariki, hususan wananchi wa Uvira ambao wameathirika hivi karibuni, ni kwenda kazini, kuimarisha mapato yetu na hivyo kutuwezesha kukabiliana na hali hii ya msukosuko. Vikosi vya ulinzi na usalama vitawekwa katika maeneo yote yenye hatari ili kuzuia jaribio lolote la kuvuruga amani. Mtu yeyote atakayekiuka uamuzi huu atakamatwa.”
Upinzani umekuwa ukitaka kufanyike mazungumzo ya kitaifa yatakayo jumuisha makundi yote ya kisiasa na makundi ya waasi ikiwemo M23 ikisimamiwa na muungano wa makanisa katoliki na protestanti, jambo ambalo serikali ya tshisekedi inakataa.
Asasi za kiraia: Hatua iliyochukuliwa inaenda kinyume na katiba ya nchi
Hata hivyo hiyo jana kadinali Fridoli Ambango ameelezea umuhimu wa kufanyika mazungumzo hayo.
“Mpango huu unalenga kugusa mizizi ya mgogoro, kwenda ndani zaidi kwa kurejesha ukweli, haki na heshima ya kila binadamu. Ni jukwaa la kuwaalika wahusika wote wa mgogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na jumuiya ya kimataifa, kuunga mkono mpango huu na kuusukuma mbele.”
Asasi za kiraia hapa nchini zimezungumzia kusikitishwa kwake na hatua hiyo ya serekali na kuonya kuwa hii inaenda kinyume sio tu na katiba ya nchi lakini pia inakiuka haki za msingi za binadamu. Elodi Ntamuzinda ni moja ya wanaharakati wa mashirika ya kiraia nchini Kongo.
Jamuhuri ya kidemokrasia ya kongo inakabiliwa na migogoro sio tu ya kisiasa lakini pia vita kutoka kwa makundi ya waasi ambao wanaendelea kusonga mbele katika eneo la mashariki mwa nchi hio. Upinzani umekuwa ukilaumu serekali ya Kinshasa kushindwa kulivalia njuga suala hilo na kwamba Raisi Felix Tshisekedi anatumia njia iyo ili kutaka kusalia madarakani jambo ambalo serekali linakanusha.