Huku wanajeshi wakishuhudiwa wakishirikiana na polisi kuwadhibiti wagombea na wafuasi wa wa upinzani wakiendesha kampeni zao kuelekea uchaguzi mkuu mwakani, kero kubwa miongoni mwa wananchi ni kwamba yamkini jeshi linasimamia uchaguzi ambao ni jukumu la tume ya uchaguzi.
Kulingana na wanajamii mbalimbali visa vya wanajeshi kuwasambaratisha wafuasi wa wagombea na hata kuwacharaza fimbo sambamba na matamshi yanayotolewa na baadhi ya maafisa wa ngazi za juu za jeshi sasa vinafasiliwa kama vitisho kwa raia. Sarah Birete ni mwanaharakati wa masuala ya utawala na demokrasia.
“Ni katika mazingira gani tunatakiwa kuwaona wanajeshi kwenye barabara za miji. Tumeteseka vya kutosha kimawazo. Tutarejelea vipi utawala wa kisheria bila kutatua hali hii ya kiburi na ukaidi wa jeshi katika nchi hii?”
Museveni akosolewa, wanajeshi kushiriki kampeni za chama chake
Kulingana na wadadisi, ni kosa kubwa kwa rais Yoweri Museveni kuwachia wanajeshi kushiriki katika kampeni za chama chake pamoja na kutoa maagizo kwa wapigaji kura. Wanahoji kwa nini tume ya uchaguzi haijajitokeza waziwazi na kudhihirisha kuwa ndiyo iliyo na mamlaka katika masuala ya uchaguzi.
Yvonne Mpambara ni mdadisi wa siasa ambaye anataka ibainike kuwa taasisi za kiusalama kama jeshi zisiingilie majukumu ya zile za kiraia.
“Unawezaje kuwaruhusu wanajeshi wakupigie kampeni na kufedhehesha chama cha NRM kwa iwango hicho? Ni fedheha kubwa kwa mgombea ambaye anatetea kiti cha urais.”
Wanasheria nao wamehimiza tume ya uchaguzi kuzingatia katiba na kufahamu kuwa uchaguzi ni suala nyeti la haki za binadamu. Wanatoa angalizo kuwa pale wanajeshi wanapotoa matamshi ambayo yanakinzana na katiba ya nchi huku wakikabiliana na wagombea wa upinzani ambao wana haki ya kushiriki kampeni, ina maana kuwa nchi imo katika utawala wa kijeshi wala si kikatiba.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa chama tawala cha NRM wanasisitiza kuwa polisi wanahitaji kupata usaidizi wa jeshi katika masuala ya kuhakikisha uthabiti katika kipindi cha uchaguzi na si kwamba hii ni kinyume na katiba ya nchi, Meja mstaafu Martin Awich ambaye pia ni mwanasheria ana ufafanuzi huu.
“Kimsingi uhusika wa wanajeshi safari hii ni kudhibiti umati wa watu na usalama kwa jumla. Lakini kama kuna wanajeshi binafsi wanaoshiriki katika kampeni ni kinyume na sheria.”
Siku chache zilizopita, raia watatu akiwemo padre wa kanisa Katoliki walitekwa na watu waliodaiwa kujihami kwa bunduki huku wakiwa wameficha sura zao na za nambari za magari waliotumia.
Awali polisi na vyombo vya usalama vilikanusha kuhusika hadi hapo Jumapili jioni wakati kaimu msemaji wa jeshi Kanali Chris Magezi alipotoa taarifa kwamba walikuwa wanamshikilia padre huyo.
Matukio kama hayo ndiyo yamezidisha hofu na wasiwasi kwamba jeshi sasa limekiuka mipaka yake kwa kuwateka raia wa kawaida na kuwazuilia kwa muda mrefu kinyume na sheria halafu baadaye kuelezea kuwa watawasilishwa kwa taasisi za kisheria.
