Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Wawakilishi la Marekani inatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kibunge kati ya Tanzania na Marekani.

Ujio wa kamati hiyo umeafikiwa baada ya mwenyekiti wake, Brian J. Mast kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyeko katika ziara ya kikazi jijini Washington, D.C., nchini Marekani.

Katika mazungumzo hayo pande hizo mbili zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Marekani huku Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Wawakilishi ikipata mwaliko wa kufanya ziara hiyo nchini Tanzania mapema iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, mazungumzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kibunge na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *