KIPA namba moja na nahodha wa Pamba Jiji, Yona Amos anayetajwa kuwa yupo mbioni kutua Yanga ili kwenda kuchukua nafasi ya Khomeiny Abubakar, amevunja ukimya na kuzungumza na Mwanaspoti akisema hatma yake ipo mikononi mwa mabosi wa klabu anayoitumikia kwa sasa.

Yanga imekuwa ikihusishwa na Amosi tangu msimu uliopita alipodaiwa alikuwa hatua ya mwisho kutua Jangwani akitokea Tanzania Prisons, kabla ya kuishia kutua Pamba iliyokuwa imepanda Ligi Kuu baada ya msoto wa miaka 23, huku Khomeiny akichomolewa Ihefu na kutua kwa mabingwa hao.

Hata hivyo, kwa sasa inadaiwa kuwa Yanga, imerudi tena kwa kipa huyo ikiamini ni mtu sahihi wa kumpa changamoto Diarra Djigui kutokana na Khomeiny na Aboutwalib Msheri kushindwa kumpa ushindani kipa huyo raia wa Mali, lakini Amosi ameliambia Mwanaspoti hata yeye anazisoma stori mtandaoni.

Kipa huyo aliyepo katika timu ya taifa, Taifa Stars inayoajindaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, alisema taarifa za kutakiwa na Yanga anazisikia mitandaoni tu, kwani bado hajapokea ofa na kwamba yeye bado ni mchezaji halali wa Pamba Jiji kwa mujibu wa mkataba.

“Sitaki kuzungumzia suala la mkataba wangu na Pamba Jiji kwamba utamalizika lini, ila ninachoweza kusema mimi bado ni mchezaji wa Pamba na kama kuna ofa, basi waajiri wangu ndio wanatakiwa kufuatwa na kulizungumzia na ninawasikilizia wao kama wewe unavyosoma mtandanoni tu,” alisema.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu mkataba wa Yona na Pamba Jiji unatarajia kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu kwani alisaini miaka miwili kuitumikia msimu uliopita akitokea Prisons.

Licha ya Yona kuchomoa kiaina juu ya taarifa hizo za kurudiwa na Yanga kwa mara nyingine, lakini chanzo cha kuaminika kinasema kwamba, pamoja na watetezi hao wa Ligi Kuu na Kombe la FA kuwa na kipa bora, Djigui Diarra, klabu ina mpango wa kuongeza nguvu katika dirisha dogo la Januari.

Na hesabu zimeangukia tena kwa Amosi waliyemkosa msimu uliopita na kumchukua Khomeiny inaelezwa licha ya kubakiza miezi sita katika mkataba, huenda akaachwa kama mambo yataenda sawa kupitia dirisha dogo, huku akihusishwa na klabu yake ya zamani Singida BS (zamani Ihefu).

Khomeiny yupo mwishoni kuutumikia mkataba wake na Yanga, huku akishindwa kutoa ushindani mbele ya makipa wenzake akiwamo Msheri ambaye ndiye kipa namba mbili kwa sasa baada ya Diarra na kwamba hesabu za Yanga inataka nafasi ya Khomeiny izibwe na kipa mzawa (Yona Amosi).

“Yanga inashiriki mashindano mengi, hivyo hatuwezi kumtumia Diarra kwa kila mechi pia anachoka na anaweza kupunguza ubora wake kutokana na uchovu hivyo naamini kuongezwa kwa Yona kutatoa chachu ya ushindani na kuongeza ubora kwa Msheri ambaye tayari amejihakikishia namba nyuma ya Diarra,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kilichongeza;

“Khomeiny ameonekana kuwa na makosa mengi na kushindwa kuendana na kasi ya timu, hivyo mabosi wameamua kuzungumza naye ili kuvunja mkataba uliobaki kupisha usajili mpya kama mambo yataenda vizuri basi atakayetua atakuwa ni Yona.”

Yona ameisaidia Pamba kucheza mechi tisa kushika nafasi ya tatu nyuma ya JKT Tanzania yenye pointi 17 na Yanga yenye pointi 16 kama walionazo wababe hao wa Mwanza, akiruhusu mabao sita hadi sasa akiwa na clean sheet tatu kama alizonazo Diarra, japo Yanga imecheza mechi sita tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *