
Mwanachama wa upinzani wa Sudan Kusini ameuwawa kwa risasi nyumbani kwake katika mji mkuu wa nchi, Juba.
Wanaume wanne wenye bunduki waliingia kwa nguvu nyumbani kwa Luka Mathen Toupiny Luk huko Gudele saa nne usiku Jumamosi na kumuua mbunge huyo kwa risasi, mkewe, Nyan Akolde, aliambia gazeti la Sudan Post Jumapili. Gudele iko magharibi mwa Juba.
Mbunge huyo alikuwa amerudi nyumbani kutoka kwa sala ya jioni wakati wa shambulio hilo lilipotokea, alisema Akolde. Mathen alipelekwa hospitalini akiwa katika hali tete, lakini alifariki kutokana na majeraha yake karibu saa moja baadaye, aliongeza mjane.
Kulingana na Akolde, washukiwa wawili wamekamatwa kwa kuhusika na mauaji ya mumewe, wakati wawili wengine bado hawajakamatwa.
Sababu ya mauaji hayo bado haijajulikana.
Mathen aliwakilisha kaunti ya Cueibet katika Baraza la Majimbo, chumba cha juu cha Bunge la Kitaifa la Sudan Kusini. Cueibet iko katika Jimbo la Lakes katikati ya Sudan Kusini.