
MNA hela? Je, klabu yako inahitaji mashine mpya ili kuimarisha kikosi kupitia dirisha dogo? Kama ndio, basi usikonde, maana kuna mastaa kadhaa wa klabu za Ligi Kuu Bara ambao mikataba yao ipo ukingoni na unaweza kuwanasa kupitia dirisha dogo litakalofunguliwa Januari, 2026.
Ndio, zikiwa zimebaki takribani siku 15 kabla ya dirisha hilo kufunguliwa, kuna mastaa kibao hadi kufikia kipindi hicho watakuwa huru kutokana na mikataba yao kumalizika au mingine kuwa ukingoni na klabu zenye fedha zake zinaweza kuwabeba kiulaini tu wakielewana.
Kuna wachezaji waliobakiza miezi sita tu katika mikataba yao, muda ambao unawaruhusu kufanya mazungumzo na klabu nyingine zinazowahitaji, wakikubaliana wanaweza kutua kipindi hiki kwa kununuliwa au mwisho wa msimu kwenda bure.
Kuanzia pale Simba, Yanga hadi Azam na Singida Black Stars kuna mastaa kibao kwa sasa wapo sokoni na klabu zilizo na nia ya kuwabeba mradi wavunje benki, basi zijue zinaweza kuwapata kiulaini hasa kutokana na wengine kukosa namba za kucheza katika vikosi vya kwanza.
Ikumbukwe kuwa, timu hizo zimekuwa na kawaida ya kuchukuliana wachezaji ambapo kipindi cha dirisha kubwa msimu huu, Simba ilimchukua Jonathan Sowah kutoka Singida BS, huku klabu hiyo nayo ikawachukua Clatous Chama, Khalid Aucho na Nickson Kibabage kutoka Yanga.
Azam ilimrudisha Aishi Manula aliyemaliza mkataba ndani ya Simba, wakati Yanga ikimbeba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kutoka Simba akiwa mchezaji huru na Frank Assinki aliyetokea Singida Black Stars akitua Jangwani kwa mkopo.
Hapa kuna orodha ya baadhi ya nyota kutoka klabu hizo ambao kipindi cha usajili wa dirisha dogo au mwisho wa msimu huu, lolote linaweza kutokea ilimradi wanaowataka wawe na pesa mkononi kwani mikataba yao ipo ukingoni na kifupi ni kama wapo sokoni kwa sasa.
Watetezi hao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) na lile la Muungano, wana mastaa zaidi ya watano ambao mikataba yao ipo ukingoni na kama mabosi wa Jangwani hawatakomaa nao huenda wakaishia kuwasikia hewani iwapo watamalizana na klabu nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Yanga ni kwamba wachezaji ambao mikataba yao ipo ukingoni na kwa sasa ni kama wapo sokoni kwani lolote linaweza kuwatokea kama mabosi wa klabu hiyo hawatachangamka ni pamoja na kiungo mkongwe, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye mkataba wake umesaliwa na miezi kama sita kabla ya kufikia tamati.
Sure Boy alisajiliwa na Yanga misimu mitatu na nusu iliyopita kupitia dirisha dogo la mwaka 2021-22 kabla ya mwaka jana kuongeza tena miwili inayofikia tamati mwishoni mwa msimu huu kama ilivyo kwa straika Prince Dube aliyetua msimu uliopita kutokea Azam na kupewa miaka miwili.
Licha ya kupigiwa sana kelele za kutotumia nafasi nyingi anazopata, Dube alimaliza msimu wa kwanza na mabao 13 ya Ligi Kuu, moja tu nyuma ya Clement Mzize aliyekuwa kinara wa timu hiyo aliyefunga 14 akiwa nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 16 na kuongoza orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu.
Msimu huu amepewa nafasi ya kuongoza mashambulizi mbele ya usajili mpya, Andy Boyeli anayecheza kwa mkopo kuitoka Sekhukhune United ya Afrika Kusini na Mzize aliye majeruhi.
Pia kuna beki Kibwana Shomary aliyeongezewa mkataba mpya Julai mwaka jana unaomalizika mwisho wa msimu huu, akiwa amepoteza namba katika kikosi cha kwanza tangu ujio wa Yao Kouasi na Israel Patrick Mwenda.
Nyota wengine ambao mikataba yao ipo ukingoni Jangwani ni Farid Mussa aliyetua Yanga 2020 kisha kuongezewa mkataba mpya Julai mwaka jana unaoisha mwishoni mwa msimu huu, huku akitajwa kutakiwa na Mbeya City, japo inadaiwa mwenyewe hakati kwenda kucheza katika klabu za mkoani.
Beki Chadrack Boka aliyekuwa akishindania namba na Nickson Kibabage kwa msimu uliopita kabla ya msimu huu kuletewa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyemng’oa katika kikosi cha kwanza, naye mkataba wake upo mwishoni na lolote linaweza kutokea.
Kipa Khomeiny Abubakar aliyesajiliwa msimu uliopita kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu kutoka Ihefu (sasa Singida Black Stars) mkataba wake ukifika Januari 2026 utakuwa umebaki miezi sita, huku akitajwa kuwa mbioni kuondoka kurudi alikotoka kumpisha Yona Amosi wa Pamba Jiji.
Kwa upande wa Simba kuna wachezaji zaidi ya wanne ambao mikataba yao nayo ipo ukingoni na kama mabosi wa klabu hiyo hatawafanya mambo mapema huenda ikala kwao katika dirisha dogo linalofunguliwa Januari mwakani.
Kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu msimu uliopita akifunga 16 mkataba wake wa miaka miwili unafikia tamati mwisho wa msimu huu na lolote linaweza kumtokea kutokana na msimu huu kupoteza ufalme alionao awali mbele ya nyota wengine.
Morice Abraham ambaye kwa sasa amegeuka kuwa lulu katika Simba, alitua msimu huu akipewa mkataba wa mwaka mmoja na sasa umesaliwa na kama miezi sita, huku akianza kumezewa mate na klabu nyingine na kama mabosi wa Msimbazi hawatafanya chapu huenda wakaachiwa manyoya.
Kiungo mshambuliaji huyo mzawa alisajiliwa na kocha Fadlu Davids kabla ya kocha huyo kutimkia Raja Casablanca na alimpa mkataba huo mfupi kwa vile alikuwa hajacheza kwa muda mrefu, lakini kazi kubwa aliyoifanya kwa sasa ni wazi Simba hawatafurahia akibebwa kwenda kwingine.
Straika Steven Mukwala ni miongoni mwa wachezaji wengine ambao mikataba yao ipo ukingoni na amekuwa akitajwa kunyemelewa na klabu kutoka Afrika Kaskazini na kwa sasa ameenda katika fainali za Afcon 2025 akiwa na timu ya taifa ya Uganda na lolote linaweza kumtokea.
Winga Joshua Mutale ni mchezaji mwingine mkataba wake upo ukingoni na yupo sokoni kwa sasa kwani kama mabosi wa Msimbazi ambao walitaka kumfyeka tangu dirisha lililopita kama dili lake la kununuliwa lingetiki, wanadaiwa bado hawamuelewi, licha ya umachachari wake uwanjani.
Huu ni msimu wa pili kwa Mzambia huyo na alianza vizuri akiwa panga pangua kwenye kikosi cha Simba wakati kinaongozwa na Dimitar Pantev aliyesitishiwa mkataba hivi karibuni.
Pia kuna kiungo mkongwe Mzamiru Yassin aliyeongezewa mkataba wa miaka miwili Juni mwaka jana na sasa umesaliwa na miezi kama sita kufikia tamati, japo kikosini hatumiki sana tofauti na misimu ya mwanzoni alipotua akitokea Mtibwa Sugar 2016-2017 kisha kuongeza mkataba mwingine mwaka 2022 na kumalizika mwaka jana kabla ya kuongezwa huu unaoelekea mwishoni.
SINGIDA BS
Wawakilishi hao wa Kombe la Shirikisho Afrika wana mashine kama nne za uhakika za kikosi cha kwanza ambazo mikataba yao ipo mwishoni akiwamo Clatous Chama aliyetua msimu huu akitokea Yanga akipewa mwaka mmoja unaoelekea mwisho sawa na ilivyo kwa kiungo Khalid Aucho.
Uwezo aliouonyesha ndani ya Singida akiisaidia kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na kubeba Kombe la Kagame, unampa nafasi ya kutamaniwa na klabu nyingine, hata hivyo, Singida inapambana kumbakisha kama ilivyo kwa Aucho.
Kiungo huyo Mganda aliyepo fainali za Afcon naye alitua Singida msimu huu akitokea Yanga na kupewa mwaka mmoja unaoelekea mwishoni, huku kukiwa na taarifa kwamba Yanga inataka kumrudisha ili kuimarisha eneo la kiungo kutokana na Moussa Balla Conte ambaye alisajiliwa kuziba pengo lake, anatajwa huenda akaondolewa na Aucho kurejea katika nafasi yake.
Pia kuna kiungo mwingine kiraka anayetumika wakati mwingine kama beki wa kati, Morice Chukwu aliyetua klabuni hapo kutoka Rivers United ya Nigeria na kutolewa kwa mkopo Tabora United (sasa TRA) kabla ya kurudishwa msimu huu na kujihakikishia namba mbele ya Miguel Gamondi.
Mkataba wake nao upo ukingoni, kuna uwezekano akaibukia timu nyingine iwapo watakubaliana kimasilahi, japo sio rahisi kwa kocha Gamondi kumruhusu kuondoka kwa namna anavyomkubali.
Beki wa kati kutoka Ivory Coast, Anthony Tra Bi Tra naye mkataba wake upo mwishoni kwa sasa kwani utaisha mwisho mwa msimu na kama Singida itazubaa huenda akaibukia kwingineko huku kuna taarifa klabu inataka kumuacha amalize mkataba huo kwa sababu eneo hilo lina nyota wengine kadhaa akiwamo Chukwu, Mukrim Issa, Kennedy Juma, huku Frank Assinki akicheza Yanga kwa mkopo.
Matajiri hao wa Ligi Kuu Bara, Azam wana nyota kadhaa ambao mikataba yao ipo ukingoni akiwamo kiungo James Akaminko, Adolf Mtasingwa, Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambao itafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Akaminko kuitoka Ghana amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza tangu chini ya kocha, Youssouf Dabo na hata sasa kwa Florent Ibenge, wakati Adolf aliyeongezwa mkataba wa miaka miwili Agosti mwaka jana baada ya kuwepo kwa kelele za kuhitajiwa na Yanga ni majeruhi kwa muda mrefu.
Kwa Sopu aliyetua kwa mbwembwe Azam mwaka 2022 akitokea Coastal Union iliyocheza fainali za Kombe la ASFC dhidi ya Yanga na kupoteza kwa penalti baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya 3-3 yeye akipiga hat trick, aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja unaokamilika mwakani.
Mbali na wachezaji hao wa klabu hizo nne kubwa, pia kuna wachezaji wa klabu nyingine 12 zilizopo Ligi Kuu Bara msimu huu ambao mikataba yao ipo mwishoni na lolote linawaza kutokea, baada ya makocha wa klabu hizo akiwamo Pedro Goncalves wa Yanga kuwasilisha ripoti ya kutaka nani abaki na yupi aondoke kupitia dirisha dogo, huku akimhakikisha maisha Prince Dube.