TRAKOMA ni ugonjwa wa macho unaoweza kuzuilika na kutibika, na ukiachwa bila matibabu husababisha upofu wa kudumu. Kwa mujibu wa madaktari bingwa wa magonjwa ya macho, ugonjwa husababishwa na bakteria anayejulikana kwa jina la ‘Chlamydia trachomatis’ na huenea kwa njia ya kugusana moja kwa moja na macho au uso wa mtu aliyeambukizwa.

Inaelezwa pia kuwa, ugonjwa huo unaweza kuenezwa kwa kutumia vitu vya pamoja kama taulo au nguo chafu, nzi wanaotua kwenye macho ya mgonjwa na kusambaza bakteria kwa watu wengine.

Chanzo kingine cha kuambukizwa ni hali ya mazingira machafu sambamba na upatikanaji mdogo wa maji safi na salama. Kwa kutambua hilo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweka mikakati ya SAFE (‘Surgery’ yaani upasuaji, ‘Antibiotics’ yaani viuavijisumu, ‘Facial cleanliness’ yaani ‘usafi wa uso na ‘ Environmental improvement yaani uboreshaji wa mazingira’) ili kutokomeza trakoma. SOMA: Tupambane na ‘mtoto wa jicho’ kuyalinda maisha ya Mtanzania

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na elimu ya jamii, usafi wa mazingira na upatikanaji wa huduma za afya, mambo ambayo ni nguzo muhimu katika kupunguza maambukizi na madhara yake. Makatibu wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) wa halmashauri za Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wanaeleza kuwa jitihada kubwa zinaendelea kufanywa na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu mkoani Morogoro, Katibu wa TLB Wilaya ya Morogoro, Christopher Mkumbi anaiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza kasi ya utoaji elimu na dawa kinga kwa jamii ili kuyatokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele ifikapo 2030.

Anasema chama hicho kina wanachama zaidi ya 40. Katika maelezo yao, wengi wanabainisha kuwa, kutokuona kwao kumesababishwa na kuugua magonjwa ya surua, usubi na trakoma katika miaka ya nyuma. Mkumbi anasema miaka hiyo, elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambayo ni matende, mabusha, usubi, trakoma, kichocho, minyoo; pamoja na chanjo na dawa kinga zilikuwa hazijasambazwa zaidi vijijini.

Anasema changamoto kubwa ambazo chama hicho kinaziona kwa sasa ni hali ya watu wenye rika la kati na umri mkubwa kupata ulemavu wa kutoona. Anasema ukifuatilia na kupata maelezo yao, wanadai kuwa ulemavu huo wameupata wakiwa wakubwa na kudai unachanagiwa na presha ya macho. “Sisi kama chama bado hatuelewi changamoto ni nini na inasababishwa na nini…

Ingawa sasa hivi zipo chanjo za magonjwa haya kwani hata lile kundi la watoto wadogo ambalo miaka ya nyuma tulikuwa tunawapata na kuwapeleka shule hatulioni kwa wingi, zaidi ya kukutana na watu wazima,” anasema. Anasema chama kinajaribu kuwasiliana na wataalamu wa sekta ya afya ili kujua ulemavu wa macho ukubwani ni kutokana na presha ya macho au kuna kisababishi kingine kwani chanjo za magonjwa mbalimbali ikiwemo trakoma zinapatikana kwenye vituo vya afya nchini.

Pamoja na hayo anasema, chama kimekuwa kikitoa msaada kwa wanachama watumishi wanaopatwa na ulemavu wa macho wakiwa kazini kwa kutoa elimu na kuiandikia barua wizara husika ili mtumishi huyo aweze kubadilishiwa mfumo sambamba na kupatiwa elimu ya maandishi ya nukta nundu ili aweza kuendelea na kazi. Anasema kwa wale ambao si watumishi wa umma, chama hicho kinawashawishi waanzishe vikundi ili wanufaike na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Katibu huyo aliyepata ulemavu wa macho mwaka 2001 baada ya kumaliza elimu ya msingi baada ya kupata tatizo la presha ya macho na hakufahamishwa ilisababishwa na nini. “Mpaka sasa hivi sijawa na majibu ya moja kwa moja; presha ya macho inasababishwa na nini na kundi la watu wenye changamoto hii ni kubwa, ndio chama kinakutana nao zaidi,” anasema.

Anatoa mfano wa kijana aliyepata ulemavu huo ukubwani akiwa anasoma kidato cha nne ambapo mzazi wake alishindwa kumpatia vifaa mtambuka mapema ili eweze kuendelea na masomo japo aliendelea kwa shida hadi kidato cha sita. “Wakati ule anasoma ulikuwa ni wakati sahihi wa kumpekela shule za wasioona, akasoma na kufanya vizuri; ni kijana aliyekuwa vizuri darasani, kwa kuwa mzazi wake alikosa vifaa mtambuka na unyanyapaa ukajitokeza kwa mwanafunzi alipokuwa anasoma kidato cha sita, hakufanya vyema,” anasema Makumbi.

Katibu wa TLB Wilaya ya Ulanga, Joseph Kwanja anasema wapo wanachama 70 katika chama chao na baadhi yao wamepata ulemavu kutokana na magonjwa ikiwemo trakoma pamoja na umri mkubwa unaopunguza uwezo wa kuona lakini watoto si wengi. Kwanja anashauri serikali iboreshe upatikanaji wa dawa katika maeneo ya zahanati na vituo vya afya na kwamba madaktari wa magonjwa hayo wawe na vifaa vya kutosha vya upasuaji.

“Daktari anapokuwa na vifaa ni rahisi kwa mgonjwa wa trakoma ama magonjwa mengine ya macho kutibiwa eneo husika, endapo daktari anakuwa na vifaa vichache vya kugundua ugonjwa na vifaa vingine vya kuendelea atalazimika kumpa mgonjwa rufaa,” anasema Kwanja.

Anasema anapompa rufaa mgonjwa huyo wakati hana fedha inakuwa changamoto kwa watu wanaopatwa na ugonjwa huo unaotokana na maambukizi ya bakteria. Katibu wa TLB Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa, Innocent Hongoli anasema mbali na trakoma kuna vyanzo vingine vinahusika na ulemavu wa macho akitolea mfano wa kuzaliwa na mtoto wa jicho.

Hongoli ambaye ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Nkomolo, anasema mbali na trakoma, shinikizo la damu nalo linachangia kupofusha macho na ni muhimu kupima afya kwa mtu mzima na kwa watoto ili kutambua mapema kama kuna shida.

Pamoja na haya, anasema wagonjwa wengi wenye tatizo la kutoona waliopo vijijini wanashindwa kupata matibabu kutokana na hali duni ya kiuchumi na hawana msaada. Anashauri serikali iendelee kutoa elimu kwa maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wafadhili ili kundi hilo liweze kupata matibabu na kuwaondolea changamoto zinazowakabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *