KWA mujibu wa wataalamu wa sayansi, mtoto wa kiume anapoanza kuumbwa, korodani zake huwa tumboni na huanza safari ya kushuka chini kuanzia wiki ya nane hadi ya 15 ya ujauzito. Kuanzia wiki ya 25 na 26 hadi mtoto kuzaliwa zinakuwa zimeshafika chini katika mifuko yake. Mifuko hiyo hushuka mapema kwa ajili ya kuzipokea korodani zinaposhuka.
Bingwa wa Upasuaji wa Jumla katika Hospitali ya Aga Khan mkoani Mwanza, Dk Mathias Mwandu anasema korodani ya upande wa kushoto huwahi kufika chini, kisha njia inayoiteremsha hufunga. Anasema kama korodani ya kulia inavyochelewa kufika, ndivyo pia huchelewa kufunga. “Isipofunga vizuri hudondosha maji kutoka tumboni hadi kwenye mfuko wake (kende), matokeo yake ni kusababisha tatizo la ngiri,” anasema Dk Mwandu.
Anasema ili mzazi atambue kwamba mtoto wake ana tatizo la ngiri, atamuona anapolia korodani yenye tatizo inavimba. Mtaalamu huyo anasema hali huendelea kuwa hivyo hadi anapoanza kutembea lakini kunakuwa hakuna maumivu. Dk Mwandu anasema njia hiyo ikiendelea kuwa wazi bila kuziba hutanuka kadri mtoto anavyozidi kukua.

Kwamba, anapofikia utu uzima hukumbana na tatizo la utumbo kushuka kupitia njia hiyo. Anafafanua kuwa kutokana na ufinyu wa njia, utumbo utabanwa na kumsababishia maumivu makali. Kwa msingi huo, anahimiza wazazi kuwafanyia watoto wa kiume uchunguzi wa awali kila mara ili kubaini kama kuna changamoto yoyote inayohusiana na korodani.
“Ipo pia changamoto ya korodani moja kushindwa kushuka, na inapokaa tumboni kwa muda mrefu inaweza kusababisha saratani ya korodani,” anasema. Aidha, anasema wakati mwingine korodani inaweza kuanza kushuka lakini ikaishia njiani maeneo ya kinena, hali inayomsababishia maumivu makali katika kufanya tendo la ndoa wakati sahihi unapofika.
Anawasistiza wazazi kuwachunguza watoto wa kiume kwa kukagua mifuko ya korodani kuona kama yote imejaa au kuna iliyo tupu. Dk Mwandu anasema: “Wakati mwingine zinaweza kufika kwa ufasaha katika mifuko yake lakini zikawa hazikui, hivyo kijana hataweza kubalehe kwa sababu zinakuwa hazina uwezo wa kufanya kazi yake ya kuzalisha manii.”
Kuhusu hali hiyo, mtaalamu huyo anashauri wazazi na walezi kuchunguza korodani za watoto wao kama zinakuwa sambamba na ukuaji wa mtoto. Anasema kama hazikui, wawahi hospitali kwa matibabu sahihi ya kitaalamu. Mtaalamu wa Mfumo wa Mkojo wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza, Dk John Igenge anaunga mkono hoja ya wazazi, hasa mama kukagua korodani za mtoto baada ya mtoto kuzaliwa ili kuhakikisha kama zimefika kwenye mifuko yake.
Anasema kama hazipo, mtoto apelekwe hospitali kwa matibabu ya kuzishusha na kwamba, matibabu hayo yanapaswa kufanyika ndani ya miezi 18 tangu kuzaliwa. Anasema zisiposhushwa ndani ya muda huo, zitaharibiwa na joto la mwili zikiwa tumboni zilipojificha na hazitakuwa na kazi. Kwa mujibu wa Dk Igenge, kuharibika huko kunaweza kusababisha saratani ya korodani lakini pia kumfanya asipate watoto atakapokuwa mtu mzima.
Anasema: “Hii ni kwa sababu mfumo wa homoni wa kuzalisha vichocheo kwa ajili ya kazi za kiume, kama vile upatikanaji wa mbegu na kufanya tendo la ndoa unakuwa umeathirika jumla.” Anasema kwa kawaida, homoni hizo zinazalishwa katika kende na aina fulani ya seli, baada ya seli hizo kupokea taarifa kutoka kichwani.

Anasema kiafya ujazo wa homoni hizo unapaswa kuwa si chini ya desilita 3.5 sawa na lita 0.35, ikiwa chini ya hapo, mwanaume anaweza kupata changamoto kama vile kukosa hamu ya tendo la ndoa, uwezo mdogo wa kutungisha mimba na kumaliza tendo la ndoa haraka. “Tafiti zinasema anaweza hata asifikishe dakika tatu… Kadhalika anaweza kuwa anatoa mbegu lakini zisizo na nguvu ya kuzalisha mtoto,” anasema.
Dk Igenge anawashauri watu wazima pia kujichunguza na kuhakikisha afya ya korodani zao kuwa sawa kwa kuzikagua mara kwa mara, kuhakikisha kama zimeenea ipasavyo katika mifuko yake, hazijapanda juu, hazijazungukwa na maji na kama ukubwa ni ule ule wa kati ya sentimita 4 hadi 5 kwa urefu na upana wa sentimita 2.5 “Endapo zimezungukwa na maji katika mfuko wake, zikibonyezwa zinahama. Na hiyo inakuwa ni dalili ya kupata ugonjwa wa busha,” anasema.
Mtaalamu huyo anassema mtu anayehisi maumivu kwenye korodani anapaswa kuwahi hospitali na kupatiwa matibabu ndani ya saa nne hadi sita kwani upo uwezekano zikawa zinajinyonga ndani ya mfuko wake, hatimaye kufa kabisa endapo hakuna huduma yoyote ya kitabibu ndani ya muda huo. Ikitokea korodani ama zote au moja zikawa si ngumu, bali zikiminywa zinabonyea, hiyo ni dalili kwamba zimekufa na baada ya muda zitasinyaa na kubaki na ukubwa kama wa gololi.
Mtaalamu huyo anasema: “Iwapo itatokea korodani moja ikafa, ile inayobaki inakuwa na uwezo wa kufanya kazi zote za kiume kama kawaida. “Lakini hapa unahitajika umakini wa kuikagua mara kwa mara hiyo moja iliyobakia kwani huenda sababu iliyopelekea ya kwanza kufa ikaua na ya pili.” Anaongeza: “Na endapo zote zitakuwa zimekufa, itampasa mwathirika kupata matibabu ya kumuongezea homoni zitakazomuwezesha tu kufanya tendo la ndoa, na si kutungisha mimba.”
Anasema Hospitali ya Bugando inazo dawa za aina mbalimbali kwa matibabu hayo ya kuongeza homoni, kulingana na chaguo au uwezo wa kifedha wa mwathirika. Baadhi ya aina hizo ni pamoja na zile za kupachika kwenye ngozi, kuchoma sindano, vidonge au za kupaka mwilini. “Muda wa kukaa nazo mwilini hutegemea na ukubwa wa dozi inayohitajika,” anasema Dk Igenge. SOMA: Washauriwa kuzingatia usalama wa watoto kwenye vyombo vya usafiri
Anatahadharisha wanaume akisema: “Njia nyingine za kulinda afya ya korodani ni kuepuka kuoga maji ya moto sana, kutovaa nguo za ndani zinazobana kupita kiasi na kuepuka matumizi ya sauna ya mara kwa mara kwani joto lake ni hatari.” Anaongeza: “Kuna wakati hasa katika msimu wa baridi kali, kende zinaweza kupanda tumboni kwa ajili ya kupata joto la mwili. “Mwanaume akiona hali hii asiogope, zitateremka zenyewe hali ya hewa itakapokuwa sawa”, alisema.