UMOJA wa Mataifa (UN) umesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na mshikamano ndani ya Afrika na duniani kwa ujumla.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres pia alisema Tanzania imezidi kuwa imara licha ya amani yake kujaribiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Guterres alisema hayo alipopokea ujumbe maalumu wa Tanzania uliowasilisha kwa na mjumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ujumbe wa Rais Samia katika ofisi za UN uliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyeongoza ujumbe wa Tanzania.

Guterres alisema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na mshikamano wa kijamii Afrika na dunia kwa ujumla.

Alisema sifa ya Tanzania ya kuwa mfano wa amani ilijaribiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu na akapongeza ustahimilivu wa nchi katika kuendeleza umoja.

Guterres alisema UN inapenda kuona Tanzania inaendelea kuwa na umoja na kuwa mfano wa kuigwa.

Alisema ni muhimu kuwa mjadala shirikishi wa kitaifa kwa lengo la kutafuta chanzo cha matukio ya vurugu ya Oktoba 29, mwaka huu na kuweka mikakati yasijirudie tena.

Guterres alisisitiza UN itaunga mkono juhudi za Tanzania ikiwa ni pamoja na wakati na baada ya kukamilika kwa jukumu la Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Tanzania kuchunguza matukio ya siku ya uchaguzi na siku chache zilizofuata.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *