Hapo ni  kwenye  mojawapo ya vituo vya afya ambapo akina mama wa jamii ya Turkana huwapeleka watoto wao kupata matibabu hasa kuhusiana na magonjwa na utapiamlo. Miongoni mwa huduma wanaopata watoto hao ni kupimwa kubaini viwango vyao vya utapiamlo na nini ambacho kinawakwaza kustawi kiafya. Wanachopewa ni dawa lakini muhimu zaidi ni vifungu vya chakula maalum kilicho na lishe. Lakini baada ya rais Trump kuvunjilia mbali shirika la USAID ambalo kwa miaka kadhaa lilikuwa likiendesha mipango hiyo ya kutoa misaada ya chakula, idadi kubwa ya watoto wanaugua utapiamlo.

Wazazi wao wanakabiliwa na hali ngumu kuweza kuwapa lishe mbadala kwani mifugo wao wengi ikiwemo mbuzi na ng’ombe walitokomea katika vipindi virefu vya kiangazi. Hata misaada ya kifedha ambayo Shirika la UNICEF limekuwa likitoa kwa wazazi wawanunulie chakula watoto wao imezidi kuwa haba. Mzazi mmoja kwa jina Hellen Etiman ni kielelezo cha wengine wengi ambao watoto wao wamekosa kustawi kimwili kutokana na hali hii licha ya kupokea misaada ya pesa na kwa bahati posho za chakula.

Walipotembelea baadhi ya vituo vya afya na lishe, wandishi habari wa Reuters walishtuka kukuta kwamba tangu mwezi Machi misaada ya chakula maalum haikuwa imewafikia walengwa licha ya serikali ya Marekani kutoa msaada wa dharura wa kifedha. Misaada hiyo ilianza kuwafikia wahanga hao mwezi Septemba na kwa ufafanuzi wa shirika la UNICEF ilichelewa kutokana na taratibu za kurejesha mnyororo wa ugavi na usambazaji uliokuwepo awali kabla ya USAID kusitisha shughuli zake.

Watoto wengi waugua utapianlo kufuatia ukosefu wa Ufadhili

Katika kipindi hicho shirika la Mercy Corps ambalo lilihusika katika usambazazi wa chakula hicho na huduma sambamba kilikusanya taarifa za watoto waathirika. Mwezi Agosti Marekani ilitoa misaada zaidi ya kifedha ya dola milioni 93 UNICEF kugharimia huduma hizo katika mataifa kadhaa ikiwemo Kenya ambayo inabeba mzigo wa kuwahudumia pia wakimbizi kutoka Somalia na Sudan Kusini.

Mkurugenzi wa Mercy Corps Melaku Yirga amefahamisha kuwa kutokana pengo la muda wa miezi ambapo chakula hicho maalum hakikufikishwa, watoto wengi waliugua utapiamlo na wengi wakakosa kustawi ipasavyo kulingana na umri wao. 

Njaa kali kutokana na kukatwa kwa misaada kwawaathiri wengi Kaskazini mwa Kenya
Mashirika ya misaada yasema kutokana na pengo la muda wa miezi ambapo chakula hakikufikishwa kwa waathirika, watoto wengi waliugua utapiamlo na wengi wakakosa kustawi ipasavyo kulingana na umri wao. Picha: dapd

Anapougua utapiamlo kwa muda mwa miezi kadhaa bila kupata chakula hicho maalum, mtoto hukosa kustawi na kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa mbalimbali ambayo humdhoofisha zaidi. Hata ubongo wake kuathirika kwani pia hana kinga tosha mwilini. Kwa wengi ina maana kuwa wamo hatarini kufariki na hata  matibabu yakianza tena watachukua muda mrefu kuwa katika hali bora ya ustawi na ni suala la bahati na sibu kwa maisha yao.

Rais Trump alilalamika kuwa Marekani hubeba mzigo mzito wa utoaji misaada na alitaka mataifa mengine tajiri nayo kuchangia. Nchi hiyo inasema mwaka huu pekee imetoa ufadhili wa dola milioni 263 mwaka huu pekee. Mwaka 2024, ilitoa mchango wa dola milioni 991. Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Uswidi nayo yamepunguza misaada yao.

Waziri mkuu wa Marekani Marco Rubio mara kadhaa amekanusha kwa wanahabari kwamba kukatizwa kwa misaada ya chakula kulisababisha vifo. Lakini akaongezea kuwa wanazingatia kutoa misaada kwa zile jamii ambazo kwa kiwango kikubwa zinakumbwa na uhaba wa chakula hasa kwa watoto.

Wizara ya Afya ya Kenya haijatoa tamko kuhusiana na msimamo wa Marekani wa kuzitaka nchi kuwajibikia afya na lishe ya raia wake hasa watoto wa chini ya miaka mitano. Kulingana na takwimu, angalau watu 179,000 wanakabiliwa na hali ngumu ya uhaba wa chakula nchini Kenya, idadi kubwa ikiwa katika eneo kame ya Turkana. Ilikadiriwa kuwa watoto 87,200 walio chini ya miaka mitano katika eneo la Turkana wanahitaji matibabu ya dharura kutokana na madhara ya utapiamlo. Huduma hizi zinahitaji kutokwa kufikia mwezi Aprili mwaka ujao wa 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *