Hii ni orodha ya baadhi ya wachezaji wa Kiafrika waliovuma katika ligi kubwa za Ulaya hivi karibuni:

Ligi Kuu ya Premia – Uingereza

Mohammed Salah – Liverpool; Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 aliingia kama mchezaji wa akiba na kutumia nafasi yake kwa kutoa pasi ya bao la pili kwa Hugo Ekitike katika mechi dhidi ya Brighton.

Salah aliachwa nje ya kikosi cha Liverpool katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan mnamo siku ya Jumanne, baada ya kulalamika juu ya kuachwa nje ya kikosi na kocha Arne Slot kufuatia sare na Leeds.

Hiyo ilikuwa mara ya tatu mfululizo kuachwa benchi, na kauli yake kali kwamba “ametupwa chini ya basi” imeibua tetesi kuwa huenda akaondoka Anfield Januari.

Calvin Bassey – Fulham;  ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Fulham. Beki huyo raia wa Nigeria alifunga bao katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Burnley.

Bao lake la kichwa dakika ya 31 lilikuwa la kwanza tangu mechi ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United mnamo Machi. Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Fulham ugenini Turf Moor tangu mwaka 1951.

Ibrahim Sangare – Nottingham Forest ni kiungo wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Alifunga bao la mwisho katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham.

Sangare alifunga bao dakika ya 79 kwa shuti kali lililogonga mwamba na kuingia wavuni. Bao hilo lilikuwa la pili kulifunga msimu huu na lake la kwanza baada ya mechi saba, likiisaidia Forest kuweka hai matumaini ya kusalia ndani ya Ligi Kuu ya England.

Ligi Kuu ya Uhispania – La Liga

Akor Adams na Chidera Ejuke wanaoichezea klabu ya Sevilla. Raia hao wa Nigeria walisherehekea kujumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa cha Nigeria kitakachoshiriki michuano ya AFCON kwa kufunga mabao katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Real Oviedo.

Adams alifungua ukurasa wa mabao dakika ya nne huku mwenzake Ejuke akikamilisha karamu kwa kufunga bao dakika ya 89.

Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga

Mohamed Amoura – Wolfsburg; Amoura alifunga kwa mara ya pili mfululizo katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Alipiga shuti baada ya krosi ya Christian Eriksen kukosa mwelekeo na kufikisha mabao sita na kutoa pasi mbili zilizochangia kupatikana kwa mabao msimu huu wa Bundesliga.

Algeria | Mohamed El Amine Amoura
Mchezaji wa timu taifa ya Algeria ni miongoni mwa wachezaji watakaomulikwa wakati wa majukumu ya kitaifa.Picha: Billel Bensalem/APP/NurPhoto/picture alliance

Ramy Bensebaini – Borussia Dortmund: Beki huyo raia wa Algeria alifunga bao pekee la Dortmund katika sare ya 1-1 dhidi ya Freiburg. Baada ya Serhou Guirassy kukosa nafasi kadhaa, Bensebaini alifunga dakika ya 31 kwa shuti la karibu kufuatia mpira wa kupokea pasi nzuri kutoka kwa Yan Couto.

Ligi Kuu ya Ufaransa – Ligue 1

Himad Abdelli na Harouna Djibirin wanacheza katika klabu ya Angers nchini Ufaransa.

Abdelli, anayechekea timu ya taifa ya Algeria alifunga penalti ya mapema wakati Djibirin wa Cameroon akiwapa uongozi wa mabao mawili dakika ya 85 katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Nantes. Mabao hayo ni yao ya pili msimu huu wa Ligue 1.

Abidjan 2024 |AFCON
AFCON itakayofanyika nchini Morocco itarajiwa kuwa jukwaa la kuonyesha vipaji vya wachezaji .Picha: Kim Price/CSM/ZUMA/picture alliance

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON itaanza Disemba 21, 2025 na kukamilika mnamo Januari 18, mwaka 2026. Michuano hiyo itakayofanyika nchini Morocco itarajiwa kuwa jukwaa la kuonyesha vipaji vya wachezaji wanaocheza Ulaya na vingine vingi, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona nani atakayeibuka shujaa wa soka barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *