WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Ruanda -Idiwili mkoani Songwe unaotekelezwa na wakandarasi wanawake waliopata fursa kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilometa 20 na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 45.3, wamepewa wanawake hao kupitia Umoja wa Wakandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) ili kuonesha uwezo wao na kama wataifanya vizuri, watapewa pia miradi mingine.
Ulega amesema kwa muda mrefu wanawake walikuwa wakitumika zaidi katika shughuli za kusafisha barabara lakini Rais Samia aliamua kufanya uamuzi wa kimkakati ili wanawake sasa wafanye kazi kubwa zaidi na zenye kipato zaidi. “Ninawaomba fanyeni kazi akinamama, rais anatambua mchango wenu na hawa wananchi wanataka kuiona barabara yao inakamilika kwa wakati ili kusudi waweze kuitumia kwa ajili shughuli za maendeleo,” alisema.
Ulega ambaye amekuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, alieleza kufurahishwa na kasi yao na aliwahakikishia kuwa Rais Samia anatambua mchango wa wakandarasi wanawake na ndio maana ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kujenga barabara hiyo.
Ulega amesisitiza suala la fursa za ajira kwa vijana wa eneo hilo ambalo mradi unatekelezwa na kufurahishwa na utoaji wa ajira kwa mradi huo kwa vijana na kuwataka kutolifanyia mchezo agizo hilo.
“Kama wapo vijana wanaoweza kufanya kazi lazima wapewe kazi za kufanya, ni muhimu sana wakimaliza kufanya kazi muwape vyeti vya kuonesha kuwa walifanya kazi hizo ili kazi zingine zinapokuja wajulikane kwamba hawa waliwahi kufanya kazi,” aliongeza Ulega. Kwenye suala la uwezeshaji vijana katika ujenzi, Ulega alisema msisitizo wa serikali ni kuhakikisha wanafanya kazi si za vibarua tu bali pia kupitia kampuni ndogo zinazoweza kupewa kazi za ujenzi.
Amewataka mameneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Songwe na Mbeya, kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi hao na kutokuwepo kwa makosa madogo madogo ili ujenzi wa barabara hiyo uende kwa kasi na kukamilika kwa wakati uliokusudiwa. Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga alimuomba waziri huyo kuwa wakandarasi hao wapewe kazi ya kukamilisha kilometa 79 zilizobakia endapo watakamilisha kipande cha kilometa hizo Agosti 20, 2026.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania, Judith Odunga alisema ujenzi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Sh bilioni 45.3. SOMA: Wakandarasi Tanga watakiwa kumaliza kazi kwa wakati
