
Katika tamthilia za kihistoria za Kituruki, The Ottoman ama kwa lugha ya kituruki ‘Kurulus Osman’ ni moja ya kazi inayoelezea historia ya nchi hiyo na imekuwa ikipendwa zaidi na mashabiki mbalimbali ulimwenguni.
The Ottoman si tu hadithi ya kuasisiwa kwa Dola ya Ottoman, bali pia imekuwa daraja la kukutanisha wasanii nje ya kamera.
Ipo mifano ya waigizaji kwenye tamthilia hiyo ambao baada ya kucheza kwenye Ottoman wakawa wapenzi na baadaye kuoana, Jakutay Bey (Çağrı Şensoy) askari mtiifu wa kiongozi wa kabila la Wakayi, Osman Bey aliigiza kumuoa Aygul Hatun(Buse Arslan).
Kuigiza kama mke na mume kwenye tamthilia hiyo kuliwafanya wahamishie mapenzi yao hadi kwenye maisha halisi, ilidaiwa wawili hao walipoigiza tu moja kwa moja walizama penzini na mwaka 2023 wakafunga ndoa rasmi na sasa wamebarikiwa mtoto mmoja.
Sio tu tamthilia hiyo lakini ni kama umekuwa utaratibu wa waigizaji wa Kituruki wengi wanapokuwa kwenye seti pamoja kwa muda mrefu wanahamishia hisia zao kuwa kweli na baadaye wanaoana.
Unamkumbuka Abidin Bey wa kwenye tamthilia ya Golden Boy, aliyekuwa rafiki wa karibu wa Ferit Korhan, humo aliigiza kama mwanaume aliyempenda Suna mtoto wa kwanza wa Kazim Aga baada ya kuigiza pamoja baadaye wakawa wapenzi kweli na mwaka jana walioana.
Sasa achana na mifano hiyo moja ya simulizi zinazovutia zaidi ni ile ya Faruk Aran (Alaeddin Bey) na Belgin Şimşek, (Gonca Hatun). Wawili hawa ambao waliingia katika mioyo ya watazamaji kama wapenzi wa kwenye tamthilia, hatimaye waliibuka kuwa wapenzi wa kweli katika maisha yao halisi.
Katika tamthilia hiyo Alaeddin Bey na Gonca Hatun waliigiza kama sehemu ya kizazi kipya kilichokuwa kinajengwa kuendeleza misingi ya Dola ya Ottoman. Uigizaji wao haukuwa wa mapambo pekee, bali ulikuwa na uzito wa kihistoria, kisiasa na kimaadili.
Alaeddin Bey aliigiza kama mtoto wa Osman Bey, mwanzilishi wa kizazi kipya cha Ottoman,Kiongozi anayejengwa si kwa upanga pekee bali kwa akili, elimu na hekima
Yalivyoanza
Wapenzi hao bado hajafunga ndoa na hivi karibuni waliwahi kusema wako mbioni kufunga pingu za maisha ili wawe rasmi mke na mume.
Kama ilivyo desturi ya tamthilia za kihistoria, waigizaji hupitia mafunzo ya kina kuanzia historia ya wahusika wao, mafunzo ya mapigano kama kutumia panga, mishale na kutumia farasi, hadi kujenga uhusiano wa kihisia unaoendana na simulizi. Hapa ndipo safari yao ya pamoja ilipoanza.
Walipokuwa wanaigiza walilazimika kujenga ukaribu wa kihisia ili kuwasilisha hadithi ya mapenzi yenye uhalisia. Kazi hii ya pamoja iliwaweka karibu zaidi kuliko walivyotarajia.
Watazamaji wengi waligundua haraka kolabo yao iliyokuwa ya kipekee kati ya Alaeddin Bey na Gonca Hatun. Macho yanayosema zaidi ya maneno, mazungumzo yenye hisia, na namna walivyoshirikiana kwenye matukio na changamoto yalionyesha uhalisia uliovuka mipaka ya uigizaji wa kawaida.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa burudani nchini Uturuki, hii ilitokana na heshima waliyojengeana, mawasiliano mazuri na muda mrefu walioutumia pamoja, takribani miaka saba kwenye kamera.
Licha ya kuigiza kama wapenzi wawili hao hawakuwahi kuharakisha kuweka wazi mahusiano yao. Kwa muda mrefu, walionekana tu kama wafanyakazi wenzao wenye ukaribu mzuri.
Hata hivyo, ishara zilianza kuonekana kupitia picha chache walizoshirikiana nje ya seti, pamoja na maneno ya heshima waliokuwa wakitumia kuelezea kila mmoja kwenye mahojiano.
Hatimaye, ilidhihirika kuwa uhusiano wao haukuwa wa kamera pekee, hivi karibuni waliweka wazi namna wanavyoweza kutenganisha kazi na mambo yao binafsi na namna tamthilia hiyo ilivyowakutanisha pamoja kila mmoja.
Wawili hao
Sasa Alaeddin ambaye ni Faruk Aran alizaliwa Machi 23, 1995 katika mji wa Izmir Uturuki ni mwigizaji wa televisheni na pia amecheza kwenye tamthilia nyingi kabla ya umaarufu mkubwa.
Alianza safari yake ya sanaa akiwa shule ya upili, akipenda sana uigizaji, na baadaye akasomea mafunzo ya maigizo katika Chuo cha Haliç University Conservatory sehemu ambayo ilimpatia ujuzi imara wa kitaaluma.
Faruk alianza kupata nafasi kwenye televisheni tangu mwaka 2018, akitokea kwenye kazi ndogo kama (Arka Sokaklar)
(Leke), (Iste Bu Benim Masalım), (Destan) na (Al Sancak) na nyinginezo.
Jaribio lake kubwa kabisa la kukua kwenye tasnia ya uigizaji na umaarufu ni tamthilia ya The Ottoman, ambapo anaigiza kama mhusika mwenye busara, jambo lililozidi kumfanya awe miongoni mwa vipaji vinavyotazamwa kwa sasa.
Kwa upande wa Gonja Hatun (Belgin Şimşek) alizaliwa Desemba 10, 1996 kwenye jiji la utajiri la Istanbul, Uturuki ni
muigizaji mchanga aliyeingia kwenye uigizaji mwaka 2021, baada ya kumaliza mafunzo ya uigizaji katika Chuo cha Sadri Alışık Cultural Center, moja ya vituo maarufu vya mafunzo ya sanaa ya maigizo Uturuki.
Baadhi ya kazi alizofanya Gonja kabla ya kucheza kwenye Ottoman ni Benim Hayatım (2021), Yasak Elma (2022) Canım Annem (2022) na Dünya Bu (2023).