KIUNGO wa zamani Yanga, Stephane Aziz KI amesema anaiona nafasi kubwa ya beki Yao Kouassi katika kikosi hicho.

Yao maarufu kwa jina la Jeshi, alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja, hali iliyomfanya kukaa nje kwa muda kiasi cha jina lake kutolewa katika usajili wa kikosi cha Yanga kwa msimu huu 2025-2026, lakini sasa amepona na anafanya mazoezi huku ikielezwa kuna mpango wa kumuingiza dirisha dogo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz amesema anamfahamu vyema beki huyo na mpaka sasa hakuna mtu ambaye anaweza kumweka nje.

Amesema kuwa, bado anaiona nafasi yake Yanga, licha ya kwamba ametolewa katika usajili wa dirisha lililopita ili aimarike kwanza.

“Siwadharau waliopo kwani wanaendelea kufanya kazi nzuri, ila haiwazuii viongozi wa Yanga kumrejesha Yao kazini kwa sababu ni beki bora sana.

“Ujue Yao ni mchezaji mkomavu sana, huwezi kumuona anakata tamaa, huwa nazungumza naye sana, siku zote ananiambia hawezi kurudi nyuma.

“Wanamuita Jeshi na maisha yake yako hivyo pia, yeye na Pacome niliwapokea Yanga na niliwaacha ASEC, hivyo kwangu wale ni familia.

“Kwa sasa namwona yuko fiti sana na moja kati ya kitu ambacho wachezaji tunaogopa ni majeraha ya muda mrefu kwani yanarudisha malengo na nafasi zetu nyuma.

“Viongozi wa Yanga wamemuacha mpaka sasa wanajua umuhimu wake hawawezi kukubali kumpoteza kirahisi na akirudi mashabiki watafurahi kwani najua amejipanga sana muda huu aliopata wa kupumzika.”

Yao amecheza mechi saba msimu uliopita kati ya 26 ambazo Yanga ilicheza katika Ligi Kuu Bara, huku akiwa hana rekodi ya kufunga bao wala kutoa asisti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *