
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo ameitaka Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) kulinda kwa kuweka usalama wa mfumo wao wa fedha kidijitali ili usiwe chanzo cha kuwaumiza wateja na kuleta changamoto zinazoweza kuepukika.
Benki hiyo ilizinduliwa rasmi Aprili, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa na lengo la kuwanufaisha wanaushirika na wakulima nchini kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu kutokana na kada hiyo kutokopesheka kirahisi kwenye benki nyingine za kibiashara, ambapo ilianza na mtaji wa Sh50 bilioni.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma za kifedha kidijitali za benki hiyo Desemba 15, 2025 jijini Dodoma, Chongolo amesema ili kuleta tija kwenye mfumo huo ni wajibu wa benki hiyo kulinda mifumo yake ili isiwe chanzo cha kuwaumiza wakulima.
”Teknolojia ni kubwa na pana inahitaji umakini na ulinzi wa kina ili msitoe mwanya kwa wajanja kuuingilia mfumo wenu wa kidijitali hakikisheni mnalinda fedha kupitia mifumo ili msilete changamoto zinazotia hasara inayoepukika,” amesema Chongolo.
Amesema benki hiyo ni ya kimkakati kwa serikali kwa ajili ya kuwawezesha wanaushirika na wakulima hasa katika eneo la mikopo ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakopesheki kwenye benki nyingine za kibiashara, lakini sasa wanakopesheka kwa riba nafuu.
Ameipongeza benki hiyo kwa kuanzisha huduma za kifedha kidijitali hali itakayowawezesha wakulima kupata huduma za kibenki kwa kutumia simu zao za mkononi bila kufika benki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah amesema benki hiyo imejiwekea lengo la kuwafikia wateja milioni 10 ifikapo mwaka 2030 idadi ambayo haijafikiwa na benki yoyote nchini.
Amesema mpaka sasa watu waliofungua akaunti kwenye benki mbalimbali nchini hawajafika milioni sita, lakini benki hiyo imejipanga kufikia wateja milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitano.
”Tunataka wateja wetu wapate huduma za kibenki bila kufika benki kwa kutumia huduma za kidijitali kwenye simu zao za mkononi wakiwa majumbani kwao, tunataka kila mwananchi awe na huduma hii ambapo anaweza pia kupata mikopo kwa kutumia Coopesa,” amesema Ng’urah.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Benki ya Coop ndiyo ya kwanza nchini yenye makao makuu yake jijini Dodoma na inakuwa kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Amesema benki hiyo inakuwa kwa kasi na kuzipita benki nyingine kubwa zilizoanza muda mrefu kwa kuboresha huduma zake na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa makundi ya wanaushirika, wakulima na vijana wanaojishughulisha na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.