
Waasi wa M23/AFC wanaoungwa mkono na Rwanda, wanadai kuwakamata mamia ya wanajeshi wa Burundi, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati huu vita vikiendelea jimboni Kivu Kusini.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Madai ya waasi haya, yamekuja, baada ya wiki iliyopita, kuuteka mji wa Uvira ambao unapakana na nchi jirani ya Burundi.
Kitendo hiki kimeikera serikali ya Marekani, ambayo kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje, Marco Rubio, inailaumu Rwanda kwa kukiuka mkataba wa Washington wa Desemba 4, uliotiwa saini kusitisha vita hivyo, kati ya rais Felix Thisesekedi na Paul Kagame.
Gavana wa M23 katika jimbo la Kivu Kusini Patrick Busu Bwa Ngwi, amedai kuwa, wanajeeshi hao wa Burundi waliokamatwa watarejeshwa katika nchi yao.
Mpaka sasa, serikali ya Burundi ambayo kwa miaka mingi ina wanajeshi wake nchini DRC, haijazungumzia madai hayo ya M23, huku ikiendelea kufunga mpaka wake na nchi hiyo jirani.
Hali Mashariki mwa DRC hasa Kivu Kusini, imeendelea kuwa ya mashaka baada ya waasi hao kuuteka mji wa Uvira na sasa wanatishia kusonga mbele zaidi.
Rwanda kwa upande wake inailamu DRC na Burundi kwa kuvunja mkataba huo, kwa madai ya kuendesha operesheni ya kijeshi kuwalenga watu wa kabila la Banyamulenge.