Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban ametahadharisha kuwa, hatua yoyote ya Umoja wa Ulaya ya kutwaa milki na fedha za Russia zilizozuiliwa bila idhini ya Budapest ni kukiuka sheria za Ulaya na itakuwa sawa na “tangazo la vita.”

Orban amesema maafisa wa EU wanafanya juu chini kuzuia mali za Russia zilizozuiliwa kwa “kuipuuza Hungary” na “kunajisi sheria za Ulaya mchana kweupe,” jambo ambalo anasema ni sawa na “tamko la vita.”

Ameishutumu Brussels kwa kuchochea mzozo huo, akiongeza kwamba Hungary “haitahusika” katika kile alichokiita mpango “uliopotoshwa”.

EU ilipiga kura wiki iliyopita kuzuia fedha za Benki Kuu ya Russia kwa muda usiojulikana, ikitumia mamlaka ya dharura kukwepa makubaliano ya pamoja licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama.

Hivi karibuni, Orban alionya pia kuwa, tishio la kuzuka Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia linazidi kuongezeka na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa ifanye kila iwezalo kulizuia.

Kwa mujibu wa maafisa wa Hungary, “Waliberali wa Ulaya wanaounga mkono vita” wanakwamisha kufanyika mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Russia ili kuhitimisha vita huko Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *