Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amelaani vikali kuendelea kwa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, akiashiria mashambulizi ya mabomu yanayoendelea kufanywa na Wazayuni na kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu.

Baghaei amesema mashambulizi yanayoendelea dhidi ya Gaza, pamoja na vikwazo vya kuingia kwa misaada ya kibinadamu katika enei hilo, ni uhalifu mkubwa unaohitaji hatua za haraka na madhubuti kutoka kwa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa.

Amesisitiza kwamba, taasisi za kimataifa zina jukumu la kusimamisha uhalifu huo na kuwashtaki wale waliohusika na uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari.

Akirejelea azimio la hivi karibuni la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Baghaei amebainisha kuwa, azimio hilo linasisitiza wajibu wa mataifa yote, chini ya Kifungu cha 1 cha Mikataba ya Geneva ya 1949, kuhakikisha kuheshimiwa kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Amelaani vikali ukiukwaji wa sheria za kibinadamu unaokaririwa na unaofanywa waziwazi na utawala wa Israel, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na mauaji ya kimbari, na kusisitiza hitaji la haraka la kukomesha kile alichokiita mapuuza ya utawala huo pandikzi kwa sheria.

Baghaei amesema jamii ya kimataifa, inayoongozwa na Umoja wa Mataifa, ina wajibu wa kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kukomesha uhalifu wa Israel na kuwawajibisha wahusika.

Baghaei amesema Marekani na nchi zingine zinazoipa Israel silaha na usaidizi wa kisiasa zinashiriki katika uhalifu wa utawala huo huko Palestina, Lebanon, na Syria zinazokaliwa kwa mabavu.

Ameongeza kuwa licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na Lebanon, lakini Israel inaendelea kufanya uhalifu wa kikatili dhidi ya mataifa hayo mawili kutokana na usaidizi usio na kikomo wa Washington na kutochukua hatua kwa wadhamini wa makubaliano ya usitishaji mapigano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *