Mmoja wa viongozi waandamizi wa harakati ya HAMAS amemtaka rais wa Marekani Donald Trump kuachana na sera ya Washington ya Israel Kwanza, akisema kuwa, hata wafuasi wa Trump kama vile MAGA sasa wanaiona Israel ni mzigo unaodhuru maslahi ya Marekani.

Akizungumza na Drop Site huko Doha mji mkuu wa Qatar, Khalid Mash’al amesema kwamba, hata kundi la “Make America Great Again” (MAGA) la wafuasi wa Trump sasa linaiona Israel ni mzigo wa kimkakati na inayaletea madhara maslahi ya Marekani.

“Kwa bahati mbaya, moja ya matatizo na utawala wa Marekani ni kwamba unayapa kipaumbele maslahi ya Israel kuliko maslahi ya Marekani,” amesema na kuongeza kuwa: “Hata watu wa Trump —MAGA— waligundua zamani kuwa Israel ni mzigo kwao, inakwamisha mambo na kudhuru maslahi ya Marekani.”

Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS pia amesema kwamba, kama Marekani ingeilazimisha Israel kuondoka katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu, Hamas na watu wa Palestina nao wangekubali kuchukua hatua inayofanana na hiyo. Aidha amesema kuwa, “Jaribio lolote la kuanzisha mamlaka isiyo ya Palestina ndani ya Ukanda wa Ghaza halikubaliki kabisa na litashindwa tu.” 

Amesema: “Mamlaka yoyote isiyo ya Palestina — yaani mamlaka ya kigeni au vikosi vya kigeni ndani ya Ghaza — itachukuliwa na Wapalestina kama ni uvamizi na lazima vita vya kuikombia Ghaza vitaendelea.” 

Mazungumzo hayo yamekuja baada ya takriban miezi miwili tangu kuanza utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Ghaza. Ametoa matamshi hayo katika hali ambayo, Marekani inapanga kutekeleza kile kinachodaiwa kuwa kupelekwa Kikosi cha Kimataifa cha Utulivu huko Ghaza, ikiyashinikiza mataifa ya Waislamu, kuchangia wanajeshi wa kikosi hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *