Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kwamba, Iran haijawahi kwenda kinyume na ahadi zake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, akisema kwamba Marekani ndiyo iliyoyachana na kuyatupa makubaliano hayo kwenye debe la taka.

Sergei Lavrov amesema katika mahojiano na Mtandao wa Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: “Nchi za Ulaya na Magharibi zilijaribu kuilaumu Iran kuwa ndiyo iliyohusika na kusambaratika JCPOA kutokana na uadui wao tu kwani Iran haikuwahi kukiuka hati hiyo.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amesema: “Mwaka 2018, Marekani ilitangaza kwamba haitafuata tena uamuzi huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hivi sasa, utaratibu mzima wa kimataifa kuhusu Iran uko katika mtihani mkubwa, na kuhusu JCPOA, ni lazima isemwe kwamba makubaliano hayo yalitupwa kwenye takataka na Marekani. Kisha Magharibi, hasa Wazungu, waliifuata Marekani kuyatupa makubaliano hayo na halafu wakaanza kuisingizia Iran.”

Aidha amesema kwamba, nchi yake inawasiliana na serikali ya Marekani kuhusu suala la Iran. Amesema: “Tunashirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tuna njia za kuwasiliana na serikali ya Marekani. Ulaya haitaki kuwasiliana nasi. Wote wana mawazo potofu. Hilo lakini ni chaguo lao. Hatuwaingilii. Hatuna mengi ya kujadiliana na viongozi wa Ulaya wa namna hii, lakini tunawasilisha mbinu zetu kwa Wamarekani kuhusu jinsi ya kurekebisha hali ya hivi sasa inayohusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Kuhusu uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran kwa kushirikiana wa Marekani, Sergey Lavrov amesema: “Tulilaani mashambulizi hayo, ambayo hayakuwa na uhalali wowote, na hadi sasa hakuna ushahidi thabiti uliotolewa na Wakala wa Kimataifa la Nishati ya Atomiki kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran. Hata hao Waisrael na Wamarekani nao hawana ushahidi kwamba Iran ilikiuka makubaliano hayo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *