
Kundi la waasi wa M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda limewakamata mamia ya wanajeshi wa Burundi wakati wa mashambulizi yake ya hivi punde mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, afisa wa kundi hilo amesema, huku mapigano yakiendelea mashariki mwa DRC.
Wiki iliyopita M23 waliingia katika mji wa kimkakati wa Uvira karibu na mpaka na Burundi, chini ya wiki moja baada ya marais wa Kongo na Rwanda kukutana Washington na Rais wa Marekani Donald Trump na kuthibitisha kujitolea kwao kufungamana na mkataba wa amani unaojulikana kama Makubaliano ya Washington.
“Tunawashikilia mia kadhaa ya wanajeshi wa Burundi ambao tuliwakamata wakati wa vita, na tunanuia kuwarudisha nyumbani,” Patrick Busu Bwa Ngwi, gavana aliyeteuliwa na M23 wa jimbo la Kivu Kusini, aliuambia mkutano na waandishi wa habari karibuni.
Busu Bwa Ngwi amesema Burundi inapaswa kutuma ombi rasmi la kurejea kwao, na kwamba M23 inavitaka vikosi vyote vya Burundi “kuondoka katika eneo letu na kurejea nyumbani kwa amani.” Jana Jumatatu Burundi ambayo imekuwa na wanajeshi mashariki mwa Kongo kwa miaka kadhaa haikutoa radimali yake kuhusu taarifa hizo.
Zaidi ya watu 500,000, wakiwemo zaidi ya watoto 100,000, wamekimbia makazi yao tangu Desemba 1 kutokana na mapigano makali katika mkoa wa Kivu Kusini wa mashariki mwa DRC. Hayo yalitangazwa Jumapili na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).
Katika taarifa yake hiyo, UNICEF imesema kuwa “ina wasiwasi mkubwa” kutokana na kuongezeka kwa kasi mapigano huko Kivu Kusini na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya watoto na familia zao kukimbilia maeneo mengine ya ndani ya DRC na wengine kuvuka mipaka na kuingia katika nchi jirani za Burundi na Rwanda.
UNICEF imetoa mwito kwa pande zote zinazopigana, kuheshimu usalama wa raia na sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu.