Kundi la waasi la Harakati ya Machi 23 (M23) lilitangaza jana Jumatatu kwamba limeamua lenyewe tu kuondoa vikosi vyake katika mji wa Uvira wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambao lilidai kuwa liliuteka wiki iliyopita na kusema kwamba, hatua hiyo imechukuliwa ili kujenga imani na kutia nguvu mchakato wa amani kati yao na serikali ya Kinshasa.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Corneille Nangaa, kiongozi wa kisiasa wa Muungano wa Mto Congo (AFC) ambao ni muungano wa kisiasa na kijeshi unaoshirikiana na waasi wa M23, amesema kwamba, uamuzi huo umefuatia matukio ya hivi karibuni chini ya mchakato wa amani wa Doha, ikiwa ni pamoja na kusainiwa Mkataba wa Amani wa Doha mwezi uliopita wa Novemba.

Waasi wa M23 wameeleza nia yao ya kujenga uaminifu kwa upande mmoja kwa lengo la kuyapa nafasi kubwa ya kufanikiwa mazungumzo ya amani ya Doha ili yaweze kutoa suluhisho la kudumu la mgogoro wa DRC.

Tangu mwezi Machi mwaka huu, kumeshafanyika duru kadhaa za mazungumzo kati ya waasi wa M23 na serikali ya DRC chini ya upatanishi wa Qatar, unaojulikana kama mchakato wa amani wa Doha. Mchakato huo wa amani wa Doha umepelekea kusainiwa Azimio la Kanuni Moja mwezi Julai mwaka huu, azimio ambalo liliweka tarehe ya Agosti 18 kuwa siku ya mwisho ya kukamilisha makubaliano ya amani. Lakini tarehe hiyo imeshapita na mpaka hivi sasa hakuna makubaliano ya amani yaliyofikiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kujiondoa waasi wa M23 huko Uvira kumefanyika kwa ombi la wapatanishi. Harakati hiyo imeongeza kuwa, imechukua hatua hiyo licha ya kuweko vitendo vya uchochezi na unyanyasaji kutoka upande wa jeshi la serikali ya DRC yaani (FARDC) na washirika wao, madai ambayo yamekanushwa na jeshi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *