
Mahakama ya Ajira ya Paris, Ufaransa imeiamuru klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) kumlipa mshambuliaji Kylian Mbappe kiasi cha Pauni milioni 52.5 (Sh175 bilioni) kutokana na mishahara na marupurupu aliyodai kunyimwa kabla ya kuondoka klabuni hapo.
Uamuzi huo umehitimisha mvutano wa kisheria uliodumu kwa miezi kadhaa kati ya Mbappe na klabu hiyo ya Ufaransa, baada ya mchezaji huyo kuwasilisha kesi akidai Pauni milioni 231.5 (Sh768 bilioni) akidai mishahara na bonasi ambazo hakulipwa.
Kwa upande wa PSG ilikuwa imefungua kesi ya kupinga ikidai Pauni milioni 211 (699 bilioni) ikimtuhumu Mbappe kukosa uaminifu kwa klabu.
Katika uamuzi wake, mahakama imebaini kuwa PSG ilishindwa kulipa mishahara ya miezi mitatu ya Aprili, Mei na Juni 2024, pamoja na bonasi ya maadili (ethics bonus) na bonasi ya kusaini mkataba, ambazo zilikuwa sehemu ya mkataba wake wa ajira.
Majaji wamesema PSG haikuweza kuwasilisha ushahidi wa maandishi unaoonyesha kuwa Mbappe alikubali kuachana na malipo hayo, licha ya madai ya klabu hiyo.
“Tumeridhishwa na uamuzi huu. Hiki ndicho kilichotarajiwa pale mishahara inapokuwa haijalipwa,” amesema wakili wa Mbappe, Frederique Cassereau.
Mahakama imetupilia mbali madai ya PSG kwamba Mbappe apoteze haki yake ya mishahara aliyodai, lakini pia imekataa baadhi ya madai ya mchezaji huyo ikiwamo madai ya manyanyaso kazini, na ukiukwaji wa wajibu wa usalama wa mwajiri.
Aidha, mahakama imeamua kuwa mkataba wa Mbappe haukuwa wa kudumu, jambo lililopunguza kiwango cha fidia ambacho kingeweza kulipwa kuhusiana na kusitishwa kwa ajira au notisi ya kuvunja mkataba.
Katika taarifa yao, mawakili wa Mbappe wamesema uamuzi huo umethibitisha kuwa sheria za ajira zinapaswa kuheshimiwa hata kwenye soka la kulipwa.
“Ahadi lazima ziheshimiwe. Hata kwenye soka la kulipwa, sheria za kazi zinatumika kwa kila mtu,” imeeleza timu ya kisheria ya Mbappe.
PSG imekuwa ikidai kuwa Mbappe alificha kwa karibu mwaka mmoja uamuzi wake wa kutotaka kuongeza mkataba, jambo lililoizuia klabu hiyo kumuuza na kupata ada ya uhamisho, sawa na Pauni milioni 165.7 walizolipa walipomsajili kutoka Monaco mwaka 2017.
Mvutano kati ya pande hizo mbili ulianza mwaka 2023 baada ya Mbappe kutangaza hataongeza mkataba wake uliokuwa unaisha majira ya kiangazi 2024, hatua iliyomfanya aondoke PSG bila ada ya uhamisho na kujiunga na Real Madrid.
Baada ya uamuzi huo, PSG ilimtenga Mbappe kwenye ziara ya maandalizi ya msimu na kumfanya afanye mazoezi na wachezaji wa akademi, kabla ya kurejea kikosini baada ya mazungumzo yaliyokuja kuwa chanzo cha mgogoro huo wa kisheria.
Katika taarifa yao, PSG imesema itaheshimu uamuzi wa mahakama huku ikizingatia haki ya kukata rufaa.
“Paris Saint-Germain inaheshimu uamuzi wa Mahakama ya Ajira ya Paris na tutautekeleza, huku tukitafakari hatua za rufaa. Tunamtakia mchezaji mafanikio mema huko aliko,” imesema taarifa hiyo.