BAADA ya kumalizana na Abdallah Kulandana, uongozi wa Mbeya City uko kwenye hatua za mwisho kumalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Azam FC, Ayubu Lyanga kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

Wakati dirisha la usajili likitarajiwa kufunguliwa mapema mwezi ujao Mbeya City tayari imeanza kusajili ikimalizana na Kulandana kwa mkataba wa mwaka mmoja, Awesu Awesu ambaye wamemuomba kwa mkopo kutoka Simba na sasa wametupa ndoano kwa Lyanga.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Mbeya City kimeliambia Mwanaspoti kuwa mchakato wa kumnasa mchezaji huyo unaenda vizuri na wanaamini wakimpata wataongeza nguvu eneo la ushambuliaji ambalo limeonekana kuwa na tatizo.

“Ni kweli tupo kwenye hatua nzuri za mazungumzo ya kumnasa mshambuliaji huyo ambaye ana uzoefu mkubwa wa ligi kuu uwezo wake tunaamini utakuwa chachu ya ushindani kikosini kwetu hasa eneo la ushambuliaji ambalo limeonyesha kuwa na tatizo kwa mechi chache tulizocheza,” kilisema chanzo hicho kutoka Mbeya City kilichoongeza;

“Usajili huo unafanywa kwa mujibu wa ripoti ambayo imeonyesha kuwa na uhitaji wa mshambuliaji lakini pia tunatarajia kusajili beki ambaye pia ataongeza nguvu eneo hilo ambalo pia linapwaya.”

Mbeya City ambayo imerudi ligi kuu msimu huu baada ya msimu uliopita kucheza Championship kwenye mechi 10 walizocheza hadi sasa wameshinda mbili, sare mbili, vipigo sita wamefunga mabao saba na kuruhusu 13.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *