Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, umeipa uhalali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, hivyo kuingia katika hatua muhimu ya usikilizwaji wa hoja za msingi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa kushirikiana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, wamekumbana na kikwazo katika jitihada zao za kuzuia kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini.

Hatua hiyo imekuja baada ya mahakama kutupilia mbali mapingamizi waliyowasilisha, hivyo kufungua njia kwa kesi hiyo kuendelea kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Uamuzi wa Mahakama wa kutupilia mbali mapingamizi hayo umeipa kesi hiyo uhalali wa kuendelea kuwepo mahakamani na kuingia katika hatua muhimu ya usikilizwaji wa hoja za msingi.

Katika hatua hiyo, walalamikaji watapata fursa ya kuwasilisha ushahidi wao kuunga mkono madai yao, kabla ya walalamikiwa kutoa utetezi wao na hatimaye mahakama kutoa uamuzi kulingana na ushahidi na hoja zitakazowasilishwa.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, Baba Levo (CCM) alitangazwa kuwa mshindi wa jimbo hilo dhidi ya mpinzani wake, Zitto Kabwe wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Hata hivyo, wananchi wanne ambao ni Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali walifungua kesi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi, mbunge huyo na AG wakipinga uchaguzi huo.

Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, wanaojitambulisha kuwa wapiga kura katika jimbo hilo, wanadai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.

Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa utaratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, ambaye ni Baba Levo.

Hivyo, wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua matokeo ya uchaguzi huo.

Serikali kwa upande mmoja na Baba Levo kwa upande mwingine waliwasilisha mapingamizi ya awali, wakitaka mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo bali iitupilie mbali, wakidai kuwa imegubikwa na kasoro za kisheria.

Serikali katika pingamizi lake ilibainisha hoja tatu za pingamizi kutaka kesi hiyo ifutwe bila kusikilizwa, huku Baba Levo akibainisha hoja mbili.

Pamoja na mambo mengine, katika mapingamizi hayo wanadai kuwa kiapo cha walalamikaji kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro katika sehemu ya uthibitisho, wakidai haikuwekwa tarehe ya uthibitisho wa kiapo hicho.

Hoja nyingine wanadai walalamikaji walitakiwa kuomba mahakamani msamaha wa  malipo ya dhamana ya gharama ya kesi hata kama wana hati ya msamaha wa malipo hayo kutoka Chama cha Wanasheria (TLS).

Vilevile wanadai walalamikaji hawana mamlaka ya kupata baadhi ya nafuu kutoka kwa mahakama zinazoombwa hususan hati ya upekuzi na uhesabuji tena wa karatasi za kura.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Projestus Khayoza, jana Jumanne Desemba 16, 2025, imetupilia mbali mapingamizi hayo yote mawili baada ya kuzikataa hoja hizo za mapingamizi ya walalamikiwa.

Badala yake, Jaji Kahyoza amekubaliana na hoja za jopo la mawakili wa walalamikaji linaloongozwa na wakili John Seka, kuwa kesi hiyo ni halali, ina msingi wa kisheria na imekidhi matakwa ya Sheria ya Uchaguzi na Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi.

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Seka amesema kutupiliwa mbali kwa mapingamizi hayo ya awali ni ushindi si tu kwa walalamikaji, bali pia kwa mustakabali wa haki.

“Walalamikiwa walijaribu kutumia mbinu ya kiufundi ili kuzuia Mahakama isiangalie kiini cha madai ya ukiukwaji wa taratibu, kanuni na Sheria za Uchaguzi, lakini mahakama imesimama kidete na kuona hoja za mapingamizi zimekosa mashiko,” amesema Wakili Seka na kuongeza:

“Sasa tuko tayari kabisa kuendelea na hatua ya usikilizwaji wa shauri la msingi, ambapo tutawasilisha ushahidi madhubuti kuthibitisha madai yetu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *