
Stockholm.Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amekutana na Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden katika Kasri la Mfalme jijini Stockholm, Desemba 9, 2025, katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo mafupi baina yao, Mfalme Gustaf na Balozi Matinyi walijadili fursa za kuendeleza ushirikiano katika nyanja za biashara, uwekezaji na utalii, maeneo yanayoonekana kuwa na mchango mkubwa katika kukuza mahusiano ya pande mbili.
Katika hafla hiyo, Balozi Matinyi alikutana na Mfalme Gustaf akiwa ameambatana na Binti Mrithi wa Ufalme wa Sweden, Victoria, Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sweden, Balozi Maria Christina Lundqvist, pamoja na mke wa Balozi, Yvonne Matinyi.
Tanzania na Sweden zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria, hususani katika masuala ya maendeleo, elimu na afya, huku mkutano huo ukitajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuufungua ukurasa mpya wa ushirikiano unaolenga maslahi ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili.