Kiungo wa Manchester United, Bruno Fernandes ametoa kauli mpya kuhusu ofa aliyopokea kutoka klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia, akisema kuwa aliambiwa na viongozi wa Manchester United wanataka kumuachia aondoke baada ya ofa kubwa kutoka kwenye klabu hiyo.

Hata hivyo, Fernandes, ambaye ni nahodha wa Man United, amekataa ofa hiyo ya pesa nyingi akitaka kubakia Old Trafford.

Al-Hilal ilikuwa tayari kumlipa Bruno, Paundi 700,000 (Sh2.3 bilioni) kwa wiki, kiasi ambacho kingemfanya apate takriban Paundi 200 milioni (Sh659 bilioni) kwa mkataba wa miaka mitatu.

Manchester United pia ingepata kiasi cha Paundi 100 milioni (Sh329 bilioni) kama ingemuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, lakini Fernandes amesema kwamba ameguswa kubaki United, ambayo anadai ilikuwa tayari kumuuza.

“Huwezi kusema sina furaha, nalipwa vizuri, lakini tofauti ni kubwa. Hilo halikuwa jambo lililoniongoza. Ikiwa nitahitaji kwenda Saudi Arabia kucheza, nitaenda.

“Maisha yangu yatabadilika, watoto wangu watakuwa na maisha yenye jua, baada ya miaka sita ya baridi na mvua huko Manchester, nitakuwa nikicheza kwenye ligi inayokua, na wachezaji maarufu,” amesema Fernandes.

Fernandes ameeleza kuwa hakutaka kubadili klabu kwa sababu ya pesa, lakini amesema ameguswa na kile alichodhani kilikuwa kukosa uthamini kutoka kwa viongozi wa Manchester United.

“Kuna wakati ambao kwao, pesa zinakuwa muhimu kuliko kitu kingine chochote. Klabu ilitaka niende, hiyo iko kwenye akili yangu.

Kauli hizo zimekuja siku chache baada ya Fernandes kudai kuwa viongozi wa Manchester United walitaka aondoke kuelekea Saudi Arabia katika msimu wa kiangazi.

“Manchester United walitaka niondoke, hilo liko wazi akilini mwangu. Nafikiri hawakuwa na ujasiri kwa sababu kocha Ruben Amorim alitaka nibaki,” amesema Fernandes, akiongeza kuwa aliumizwa na namna suala hilo lilivyoshughulikiwa.

“Ningeweza kuondoka msimu uliopita na kupata pesa nyingi zaidi, na hata kushinda mataji mengi. Lakini niliamua kubaki kwa sababu ya familia na kwa sababu naipenda klabu. Lakini uaminifu siku hizi hauangaliwi kama zamani,” amesema.

“Nilikaa na familia, nikazungumza na wakala wangu na hata rais wa klabu ya Al-Hilal. Mwisho wa siku niliamua kubaki hapa,” amesema Fernandes.

Kauli hizi zinapingana na maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Manchester United, ambao walisisitiza kuwa walimwambia Fernandes kuwa ni sehemu muhimu ya mipango yao na kuwa hawakuwa tayari kumuuza.

Fernandes ameeleza pia kuwa alichukua muda kufikiria ofa ya Al-Hilal pamoja na familia yake kabla ya kuamua kubaki.

Hata hivyo, amesema alijua kuwa klabu ilikuwa vigumu kuchukua uamuzi huo kwa kuwa kiasi hicho cha fedha kilikuwa kikubwa, na hiyo ilikuwa ni tofauti kubwa tangu Cristiano Ronaldo aondoke.

“Najua klabu ilikuwa vigumu kufanya maamuzi kwa sababu ni pesa nyingi ambazo klabu haijapata tangu Ronaldo aondoke.

Najua mimi ni nahodha, ni muhimu kwao, na hata wakati mwingine nitakuwa si mzuri, lakini mimi ni sehemu ya timu,” amesema Fernandes.

Fernandes ametaja wazi ligi za nchi anazopendelea kucheza endapo ataamua kuondoka Manchester United, huku akisisitiza kuwa bado anatamani kubaki klabuni hapo muda mrefu kadri anavyohitajika.

“Ningependa kujaribu ligi ya Hispania, na pia kupigania mataji makubwa nchini Italia. Nina uhusiano mkubwa na Italia, hata binti yangu alizaliwa huko,” amesema Fernandes.

Kiungo huyo alianza kucheza soka la kulipwa nchini Italia ambapo alicheza katika Klabu za Novara, Udinese na Sampdoria kabla ya kurejea Ureno na baadaye kujiunga na Manchester United mwaka 2020 kwa dau linalokadiriwa kufika Pauni milioni 68

Fernandes amesema bado ana ndoto za kufikia mafanikio zaidi na Manchester United na kwamba atabaki mpaka atakapoamua kuondoka mwenyewe.

Kwa sasa, Fernandes bado ana mkataba na Manchester United na anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Ruben Amorim, lakini kauli zake zinaacha maswali mengi kuhusu mustakabali wake na uhusiano wake na viongozi wa klabu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *