Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka amewaonya baadhi ya maofisa habari wa Serikali kuwajengea majina viongozi wao, badala ya kuonesha kazi zilizotekelezwa na taasisi husika.

Balozi Kusiluka amesema baadhi ya maofisa hao wamejikita kutoa taarifa za viongozi wao wa taasisi, badala kutoa habari za Serikali katika taasisi zao.

“Sio wote, wapo wachache, unapokuwa kwenye taasisi, kazi yako wewe na bosi wako ni kutekeleza kazi za Serikali. Kazi ya ofisa habari wa Serikali ni kuhakikisha Serikali kwanza, viongozi wanafanya kazi ya Serikali, pia ni washauri wa Serikali.

“Msijikite kubrandi kiongozi mkasahau kuwa, kiongozi anafanya kazi ya Serikali. Sio wote, lakini kuna wengine wanajisahau, tambueni mnatakiwa kutoa taarifa za Serikali badala ya ‘brand’ ya mtu mmoja,” amesisitiza.

Ametoa onyo hilo, leo Jumatano Desemba 17, 2025 katika kikao kazi cha kitaifa cha Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais na maofisa habari wa Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Balozi Kusikula amesema Serikali imefanya maendeleo katika maeneo mbalimbali na ina mipango mingi kwa ajili ya ustawi wa wananchi iliyopangwa kutekelezwa.

“Serikali imefanya mambo mengi ya kusemwa ndani na kimataifa, lakini tutashangaa ndani ya nchi mengi hayajulikani, isipokuwa kwa watu wachache. Lakini tumebaki kuripoti matukio ya siku, ndio maana tupo hapa kuangalia tumekosea wapi na twende namna gani,” amesema.

Mbali na hilo, Balozi Kusiluka amesema kuna kero za wananchi zenye majawabu, lakini taarifa za changamoto hizo hazijawafikia wahusika kwa wakati.

Amesema ili uwe ofisa mzuri wa habari, lazima utambue cha kusema, usome na kuandika, bila kuwa na sifa hizo, utabakia kuripoti kilichotokea au unayoyajua.

Sambamba na hilo, Balozi Kusiluka amewahimiza maofisa hao kuweka utaratibu wa kutoa mrejesho kuhusu kero za wananchi zinazopatiwa ufumbuzi.

“Kuna mambo mengi yamefanyiwa kazi, lakini hatutoi mrejesho, kaeni vizuri kwenye sekta zenu ili kuhakikisha mchakato wa habari unakamilika,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Balozi Kusiluka amewataka maofisa habari hao kuwa washauri wa kimkakati wa viongozi wao, kuhusu sekta hiyo hasa namna bora ya kuwasiliana na umma.

“Kukosoa kuna hitaji heshima, si lazima umshambulie bosi wako, akigundua unaongeza kitu cha thamani kwenye kazi atakupenda. Mnapaswa kuwashauri kwa sababu ninyi ni watalaamu, simameni katika nafasi zenu, msiwe waoga,” amesema.

Amesema kuna jambo linaharibika akiulizwa, anajibu kuwa, “hata mimi nashangaa, unashaangaje wakati wewe ndio mtalaamu?”

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu amesema kikao hicho kimeandaliwa na taasisi ikishirikiana na Idara ya Habari Maelezo kikiongozwa na kauli mbiu ya: “Utu na Mawasiliano yenye Uwajibikaji.”

Machumu amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutaka kuwakumbusha maofisa hao wajibu wa kujifunza na kuutumia wingi wao kama mtaji wa Taifa katika utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwasaidia wananchi.

“Mawasiliano ya Serikali ni nyenzo ya utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo. Ofisa habari ni sehemu ya uongozi wa taasisi, mshauri wa kimkakati na daraja la heshima kati ya Serikali na wananchi,” amesema Machumu.

Amesema Serikali ina maofisa habari takribani 800 nchi nzima, hivyo haipaswi kuwa na ukame wa simulizi za manufaa zitakazowagusa wananchi badala ya kuwaachwa na maswali, bali wawe na tabasamu kila wakati linaloonesha kufurahia utendaji kazi wa Serikali yao.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kikao kazi hicho na ofisi ya Rais ni muhimu kwa sababu kinaunganisha yale yanayofanywa na maofisa habari pamoja Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *