
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan ameonya kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya Urusi na Ukraine katika Bahari Nyeusi yanaongeza vitisho vya usalama baharini na kuhatarisha kuenea zaidi ya kanda, pengine hata kuathiri kote barani Ulaya.
Katika mahojiano ya kipekee na TRT World, Fidan alisema Uturuki imeathirika moja kwa moja katika wiki za hivi karibuni, huku meli za biashara zikilengwa na pande zote mbili na ndege zisizo na rubani zikiingia katika anga ya Uturuki. Alieleza kuwa matukio kama hayo pia yameathiri mataifa jirani, ikiwemo Romania na Bulgaria.
“Tumeathirika sana katika wiki za hivi karibuni,” Fidan alisema. “Meli zimelengwa kutoka pande zote mbili, na sasa ndege zisizo na rubani zinapaa siyo tu katika pande zinazozozana lakini katika eneo letu.”
Fidan alieleza hatari ya usalama katika Bahari Nyeusi ilianza miaka kadhaa iliopita kwa kuondoa mabomu ya baharini, ambayo mengine yalifika katika mlango bahari wa Istanbul, wakati mwingine wakitatiza safari za meli katika mlango bahari wenye umuhimu wa kimkakati. “Wakati mwingine ilikuwa hatari sana kiasi cha kuzuia meli kupita kabisa,” alisema.
Aliongeza kuwa jeshi la Uturuki limekuwa likifanya kazi kwa karibu na washirika wake katika kanda, hasa Romania na Bulgaria, kukabiliana na kuongezeka kwa hatari ya safari za meli na usalama. Hata hivyo, Fidan alisisitiza kuwa uratibu wa kijeshi pekee hauwezi kutatua hali hiyo.