NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha maeneo yaliyotambuliwa wananchi wake wanapatiwa hati milki ya ardhi.
Mmuya ametoa kauli hiyo mkoani Lindi alipokutana na watumishi wa sekta ya ardhi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
“Tunataka kila mtanzania mwenye eneo ambalo limepimwa na limepangwa apewe hati yake,”amesema Mmuya.

Aidha, amewataka wataalamu wa sekta ya ardhi nchini kutekeleza kikamilifu maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapimwa.
Amesema dhamira ya Rais kupanga, kupima na kumilikisha ardhi itasaidia kuondoa changamoto za migogoro ya mipaka ikiwemo ile ya vijiji na vijiji.

Katika hatua nyingine, Naibu huyo wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezitaka ofisi za Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kutoa taarifa ya kila mwaka kuhusiana na masuluhisho mbalimbali ya migogoro ya ardhi inayoshughulikia.
“Tuharakishe kushughulikia mashauri yaliyowekwa kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya na tusikae na mashauri hayo bila sababu yoyote,” amesema.
Kikao kazi baina ya Naibu Waziri Mmuya na Watumishi wa sekta ya ardhi kimelenga kutambua juhudi za watumishi wa sekta hiyo katika kutimiza malengo ya Wizara lakini pia kufahamu changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yao.