Mbabane. Mfalme Mswati, mtawala wa kifalme mwenye mamlaka kamili, anadaiwa kumpa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, uraia wa Eswatini bila kufuata sheria ya uraia, kulingana na uchunguzi huru uliofanywa na gazeti la Swaziland News.

Kupewa uraia wa Kabila kunakuja ikiwa ni miezi michache imepita baada kuhukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama ya Kijeshi ya DRC kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na waasi wa M23, na alipatikana na hatia ya uhaini, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Swaziland News kwenye ripoti yake imedai kuwa  ushahidi wa nyaraka uliopatikana kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Eswatini unaonyesha kuwa, kufuatia agizo la Mfalme kuelekeza Bodi ya Uraia kumpa aliyekuwa Rais wa DRC uraia, Wizara ya Mambo ya Ndani iliendelea kumpa pasipoti ya kidiplomasia.

Taarifa ya gazeti hilo imeendelea kudai kuwa Jumamosi ya Novemba 29, 2025, Kabila aliondoka Eswatini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Mswati akitumia pasipoti yake mpya ya kidiplomasia ya Eswatini.

Kwa mujibu wa gazeti hilo mfumo wa Uhamiaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani unaonyesha kuwa hiyo ilikuwa safari yake ya kwanza kutumia pasipoti ya Eswatini.

Gazeti hilo limedai kuwa pasipoti mpya ya kidiplomasia aliyopatiwa Kabila, ikiwemo namba ya pasipoti, haiwezi kuwekwa wazi kwa sababu za kimaadili, kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wake.

Alipoulizwa kutoa maoni na Swaziland News Jumatano alasiri, Msemaji wa Mfalme Mswati, Percy Simelane, alisema hakuwa na taarifa kuwa aliyekuwa Rais wa DRC amepatiwa uraia wa Eswatini, lakini alifafanua kuwa watu wenye uraia wa nchi nyingi huomba uraia wa Eswatini mara kwa mara, hivyo uraia wa Kabila usingekuwa jambo la ajabu.

“Hatujui kama Kabila amepewa uraia. Tunachojua ni kwamba watu wenye uraia wa nchi nyingi huomba uraia wa Eswatini mara kwa mara. Bodi ya uraia huangalia maombi hayo, kuyakubali au kuyakataa. Ikiwa ni kweli, kumpa uraia hakutakuwa kesi ya kipekee,” alisema msemaji wa Mfalme.

Mgogoro kati ya Kabila na Rais Felix Tshisekedi wa DRC,  ulizidi baada ya Tshisekedi kumtuhumu kudumisha uhusiano na waasi wa M23.

Tuhuma hizo, pamoja na kufunguliwa kesi dhidi yake kwenye Mahakama ya Kijeshi, zinadaiwa kumlazimisha Kabila kukimbilia kujificha nchini Eswatini, ambapo baadaye alihukumiwa adhabu ya kifo bila kuwepo mahakamani.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *