Hayo yanajiri huku idadi ya vifo kwenye ajali za barabarani ikioongezeka. Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani imewaonya madereva wanaovunja sheria za barabarani kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria. Wakati kama huu wa mwaka huwa panatokea ajali nyingi sana za barabaraniambazo zinagharimu maisha ya watu.

Machakos…Kituo kikubwa cha usafiri wa magari ya umma hapa Nairobi. Wasafiri wengi wanapanga kuelekea maeneo ya vijijini ila simulizi zao zimebeba matumaini, uchovu na huzuni. Kinachopaswa kuwa safari ya kurejea nyumbani, kukutana na familia na kupata hewa ya asili, kimegeuka kuwa mtihani wa uvumilivu na ustahimilivu kwa maelfu ya wasafiri. Carolyne Omondi amekuwa na familia yake kwenye kituo hiki tangu mapema asubuhi, anaelezea kadhia yake. 

”Kwa vile hatukuweza kusafiri nyumbani huu ni mwaka wa pili sasa, tukasema tujaribu kufika nyumbani kuwasalimu wakazi kule. Tumekuwa hapa tukisubiri gari, saa nane sasa hatujapata gari.”

Kituo kikubwa cha mabasi ya kwenda mikoani cha Machakos jijini Nairobi
Mwezi wa Desemba huwa na shughuli nyingi kupindukia katika kituo kikubwa cha mabasi ya kwenda mikoani cha Machakos jijini NairobiPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kumeshuhudiwa uhaba wa magari ya uchukuzi wa umma kuliko kawaida. Asubuhi na jioni, vituo vya mabasi jijini Nairobi vimefurika watu waliobeba mizigo, watoto mikononi na macho yaliyojaa matarajio. Abiria wanasimama kwa saa nyingi wakisubiri magari ambayo hayaji kwa wakati, huku wahudumu wakitangaza safari zilizojaa au kuahirishwa bila maelezo ya kuridhisha.

Pamoja na uhaba huo, nauli zimepanda maradufu, zikiongeza mzigo kwa wananchi ambao tayari wanakabiliwa na gharama kubwa ya maisha. Safari iliyokuwa nafuu miezi michache iliyopita sasa imegeuka kuwa anasa kwa wengi. Hali ambayo imesababisha mkanganyiko kama anavyoelezea msafiri huyu. ”Kuna vituo vingi vya usafiri, kuna kituo hapa kuna kituo pale, wateja wamechanganyikiwa, magari hayapatikani.”

Safari za saa chache zimegeuka kuwa safari za siku nzima, huku uchovu ukizidi na subira kupungua. Katika kipindi cha juma moja pekee, watu 27 wamepoteza maisha yao katika ajali mbalimbali nchini Kenya. Mfululizo huu wa ajali umeilazimu serikali kuitisha mkutano wa dharura wa mashirika mbalimbali chini ya mwavuli wa Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Haki, kwa lengo la kubuni mikakati ya kudhibiti maafa yanayoendelea kuzigeuza barabara za Kenya kuwa njia za mauti.

Watu 21 walikufa wakati basi lilitumbukia mtoni kwenye daraja la Nithi nchini Kenya Julai 25, 2022
Kumekuwa na matukio ya ajali mbaya za barabarani zilizosababisha vifo vya watu wengi katika mwezi wa Desemba 2025Picha: Dennis Dibondo/AP/picture alliance

Baraza hilo linapendekeza kuanzishwa kwa mahakama za barabarani kwa ushrikiano na maafisa wa polisi na Idara ya Mahakama, ili mtu anapokutwa na makosa, aadhibiwe mara moja. Aidha, vizuizi vitawekwa barabarani kuhakikisha magari yanazingatia sheria. Andrew Kiplagat ni Mkurugenzi wa Usalama katika Mamalaka ya Usalama wa Uchukuzi nchini Kenya. ”Kila mdau awajibike, wahakikishe kuwa vidhibiti mwendo kwenye magari yao, kwa mujibu wa sheria vinapunguza kasi.”

Kwa sasa, barabara kutoka Nairobi kwenda maeneo ya vijijini zinaendelea kubeba simulizi ya taifa lenye changamoto, matumaini na wito wa mabadiliko. Watu 4,682 wamefariki dunia kwenye ajali za barabarani kwa mwaka 2025, ongezeko la asilimia tano kutoka vifo 4,479 vilivyorekodiwa mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *