
Kiongozi wa harakati ya Muqawama ya Ansarullah nchini Yemen amelaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanywa na mwanasiasa wa Marekani huku akiwataka Waislamu kote duniani kusimama imara kulinda matukufu yao.
Wito wake umetolewa baada ya Jake Lang, mgombea wa mrengo mkali wa chama tawala cha Republican katika uchaguzi wa Seneti ya Marekani, kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu wakati wa maandamano ya kupinga Uislamu yaliyofanyika Jumapili huko Plano, Florida. Kitendo hicho kichochezi kimezua hasira na ukemeaji mpana kutoka kwa Waislamu na wanaharakati wa haki za binadamu, kikitambuliwa kama uchokozi wa wazi na dharau kwa hisia za mabilioni ya Waislamu duniani kote.
Katika taarifa yake ya Jumanne, Abdul‑Malik al‑Houthi alikitaja kitendo hicho kuwa ni “jinai dhidi ya matukufu makubwa zaidi ya dini duniani,” akisisitiza kuwa ni sehemu ya “vita vinavyoendelea” dhidi ya Uislamu vinavyoongozwa na Marekani, Uingereza, utawala wa Israel na washirika wao Mashariki na Magharibi.
Kwa mujibu kiongozi wa Ansarullah, tawala hizo zinalenga kuharibu jamii za kibinadamu na kuzikoloni. Aliongeza kuwa udhalilishaji wa matukufu ya dini unaenda sambamba na “harakati pana” za kuyafanya mataifa kuwa mateka, kupora rasilimali zao na kuvamia ardhi zao.
Al Houthi amesema mfululizo wa matusi dhidi ya Uislamu, pamoja na vita laini na ngumu vinavyoendeshwa na Uzayuni na washirika wake, ni ishara ya uadui wa wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Aidha, amebainisha kuwa vitendo hivyo vinakusudia kudhoofisha nafasi ya Qur’ani Tukufu katika nyoyo za Waislamu na kuwafanya watengane na mafundisho yake, jambo linaloonyesha “chuki ya kina” dhidi ya Uislamu.
Akirejea uhalifu wa Israel dhidi ya Wapalestina na maeneo matakatifu ya Kiislamu katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu, Al Houthi amesisitiza kuwa matendo hayo, pamoja na uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel, ni uthibitisho zaidi wa uadui huo.
Amesisitiza kuwa Waislamu—serikali na wananchi, wasomi na umma kwa ujumla, wana wajibu wa kidini na kimaadili kukabiliana na nguvu za dhulma na upotoshaji zinazoongozwa na Uzayuni.
Al Houthi ameonya kuwa kutojali na kunyamaza mbele ya matusi kama haya kunawatia nguvu maadui na kunawakilisha udhaifu mkubwa wa imani, maadili na misingi ya kiroho.
Pia alikosoa ukosefu wa msimamo madhubuti wa kisiasa na kiuchumi au kutoka ulimwengu wa Kiislamu licha ya kuwa na idadi ya Waislamu takribani bilioni mbili, akisema kuwa msimamo wa wasomi na mataifa ya Waislamu kwa kiasi kikubwa umeakisi ule wa serikali zao.
Kiongozi huyo wa Ansarullah amewataka wananchi wa Yemen kufanya maandamano makubwa Ijumaa hii kulinda utukufu wa Qur’ani Tukufu na maeneo matakatifu ya Kiislamu, wakiendeleza maandamano ya kila wiki ya kuunga mkono wananchi wa Palestina.