Hekima ya wana wa dunia waliotangulia kuuishi ulimwengu, walisema: “Ukivuliwa nguo chutama.” Oktoba 29, 2025, Tanzania ilivuliwa nguo. Jitihada zote za kujisahihisha zinabeba tafsiri ya kuchutama.

Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, Bungeni, Dodoma, Novemba 14, 2025, alikiri nchi kuvuliwa nguo. Aliomba nafasi ya kujirekebisha. Aliahidi maridhiano.

Mambo kadhaa aliyafanya kutekeleza dhamira ya utayari wa maridhiano na kujisahihisha. Mosi, aliunda Tume ya Uchunguzi (Inquiry Commission), kuchunguza na kutoa ripoti ya hali halisi ya matukio ya Oktoba 29 na baada yake. Pili, aliunda Wizara ya Maendeleo ya Vijana, ili ifanye kazi maalum ya kushughulika na vijana.

Zilikuwa jitihada muhimu kutambua nafasi ya vijana katika utulivu wa nchi. Ni kundi lenye kubeba uhusika mkubwa kwenye ghasia za Oktoba 29, 2025. Vijana hawakuasisi mwamko wa kuingia barabarani, isipokuwa walijengwa na kuaminishwa, kisha wakaitikia wito. Nchi ikavuliwa nguo.

Katikati ya juhudi za kutoka mahali nchi ilipoangukia ili kuisaka kesho yenye maelewano, ustahimilivu na neema, itakayobeba mwiko wa kutorudia yaliyosababisha taifa kuvuliwa nguo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, alitokeza na kutoa matamshi yenye kutotaka nchi ichutame.

Desemba mosi, 2025, Padri Kitima, alizungumza na wanahabari na kueleza kuwa baada ya ghasia za Oktoba 29, Polisi walikwenda kwenye hospitali za Kanisa Katoliki na kuwalazimisha wahudumu wa afya, kuwapeleka majeruhi mochwari (chumba cha kuhifadhi maiti).

Ni kauli yenye kuamsha hasira na kuchokoza watu kuona Polisi Tanzania ni jeshi lisilo na ubinadamu. Majeruhi kupelekwa mochwari ni kitendo cha kinyama. Hakuna tafsiri nyingine ya alichokifanya Kitima, zaidi ya kukifungua na kukichokonoa kidonda ambacho daktari amekifunga bandeji ili kianze kupona.

Kitima ni msomi wa Theolojia. Hekima za mwana-theolojia wa Uholanzi na Padri wa Kanisa Katoliki, Henri Nouwen, zinapingana na alichokifanya Kitima. Padri Nouwen aliyeishi miaka 64 na miezi nane Karne ya 20, alipata kuandika kwamba Theolojia ni upatanisho na siyo kugawa watu.

Padri Nouwen aliandika: “One of the main tasks of Theology is to find words that do not divide but unite, that do not create conflict but unity, that do not hurt but heal.” – “Moja ya majukumu makuu ya Theolojia ni kutafuta maneno yasiyogawa watu, bali yanayowaunganisha, yasiyotengeneza mgogoro bali umoja, yasiyoumiza bali yanayoponya.”

Taifa limeangukiwa na kitu kizito. Maumivu ni makali kila upande. Kuanzia polisi waliouawa na kujeruhiwa, hadi raia waliopoteza maisha na kupata majeraha. Miongoni mwa majeraha, makovu yake wataishi nayo mpaka watakapoingia kaburini. Bila kusahau walioibiwa na kuharibiwa mali zao. Kuna mali za umma zilizoharibiwa. Wapo raia waliosakwa wakatwe vidole kwa sababu walipiga kura.

Kupita katikati ya waathirika hao ili kubainisha walio na haki kuliko wengine hiyo hayo siyo mafundisho sahihi ya Theolojia, kama alivyoelekeza Padri Nouwen. Serikali imeumizwa na ghasia za Oktoba 29, familia zimepoteza wapendwa wao. Wavuja jasho wamepoteza mali zao walizohangaikia kwa miaka. Majeruhi hawajapona majeraha. Wananchi wengi hawajapona hofu za yote yaliyotokea.

Theolojia ambayo Kitima amesoma na kufuzu ndiyo maana akawa Padri, ni somo la asili ya Mungu na imani ya kidini. Ndani ya Theolojia kuna matawi mawili, Imani na Saikolojia. Kwa muktadha huo ni sahihi kusema kuwa Padri Kitima ni mwanasaikolojia.

Oktoba 29, 2025, jinsi matukio yalivyoanza, kwa mimi niliyekuwa nafuatilia hatua kwa hatua, nafahamu kwamba askari wa Jeshi la Polisi, walikuwa walengwa. Wengi, walitafuta nguo za kiraia wavae ili kunusuru uhai wao. Katika hali hiyo na matokeo yake, Polisi waliuawa. Mpaka hapo, Kisaikolojia, tayari hisia za uadui zilishakuwapo. Jamii yako ikiwindwa iuawe, wewe utawatazameje wanaowawinda? Padri Kitima, kwa utaalamu wake wa Saikolojia, alitakiwa kufahamu athari ambayo Polisi walishakuwa nayo kutokana na matukio ya Oktoba 29, kisha angekuja na maneno ya kuunganisha na kuponya, badala ya kuchonokoa mgogoro upya.

Alichokifanya Padri Kitima, hakitibu wala hakitetei, isipokuwa kinaamsha hisia za chuki. Kinawaamsha Polisi kukumbuka wenzao waliouawa na waliojeruhiwa.

Mtu mmoja aliniandikia ujumbe unaosema: “Polisi walikuwa sahihi, wale wangewapeleka mochwari, ni wanyama. Mimi nilipona chupuchupu kukatwa kidole.”

Ipo hoja ya msomaji wangu, aliyeniandikia kupitia WhatsApp, akahoji: “Father Kitima anasema Polisi walikwenda hospitali na kushinikiza majeruhi wapelekwe chumba cha maiti, lakini ni Polisi haohao waliowapeleka hospitali, kama ni kweli, mbona Polisi walikuwa na nafasi ya kuwauaa kabla ya kuwafikisha hospitali, lakini wakawapeleka ili watibiwe?”

Kufafanua hoja yake ni kwamba nchi ilifungwa, kwa hiyo majeruhi waliopelekwa hospitali, kazi hiyo ilifanywa na Polisi. Padri Kitima anataka ionekane polisi ni wauaji. Sasa bila kupinga hoja ya Kitima, msomaji anahoji, kama kweli nia ya Polisi ilikuwa kuua watu walioshiriki ghasia za Oktoba 29, mbona waliwabeba majeruhi hadi hospitali wakiwa wazima? Ilishindikana nini kuwaua kabla ya kuwafikisha hospitali?

Upo mjadala wa amani na haki kipi kianze. Hii ni hoja ya Kitima na wengine wengi.

Swali, nyakati za machafuko, kipi huanza kutafutwa? Mnajadili haki mkiwa mnauana au mnakubaliana amani, ndipo mjadala wa haki ufuate? Hapa, napenda kuwa mfuasi wa Rais wa 40 wa Marekani, Ronald Reagan.

Katika nyakati kama hizi za Tanzania, Rais Reagan alishauri: “Peace is not absence of conflict; it is the ability to handle conflict by peaceful means.” – “Amani siyo kutokuwapo kwa mgogoro, ni uwezo wa kushughulikia mgogoro kwa njia ya amani.”

Kuundwa Tume ya Uchunguzi na wito wa maridhiano ni mpango wa kushughulikia mgogoro kwa njia ya amani. Kukataa ni kutafuta matokeo magumu. Kukabiliana na Rais ambaye anatambuliwa na dola, ni gharama ya damu za watu. Kujishusha ni wito wa Theolojia. “Kila mtu akijifanya anaona, dunia hugeuka kipofu,” alifundisha Mahatma Gandhi.

Amani haipatikani kwa shinikizo, isipokuwa kwa maelewano, aliyasema hayo mwanafalsafa Albert Einstein. Kama mwafaka wa ghasia za Januari 26 na 27, 2001, Tanzania, ulivyopatikana kwa amani na maelewano, ndivyo inavyopaswa kwa yaliyojiri Oktoba 29. Imempendekeza Mungu nichangie hekima hizi na Padri Kitima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *