Licha ya tangazo hilo, waasi wa M23, bado wako Uvira, mashariki mwa Kongo, na mapigano yanaendelea katika maeneo ya karibu.
Kulingana na vyanzo rasmi,licha ya tangazo la kundi la waasi wa M23, wapiganaji wenye silaha bado wanaonekana katika mji huo. Waziri wa Habari na Msemaji wa Serikali, Patrick Muyaya amewashutumu waasi hao kwa kuendeleza vita, siku chache tu baada ya kusaini makubaliano ya amani na kulitaja tangazo lao la kuondoka kama upotoshaji. ”Huu ni upotoshaji, kwa sababu, kama unavyojua, umewahi kusikia M23, ambao kimsingi ni mtoto wa Rwanda, wakikana kuhusika katika mchakato wa Washington. Inakuwaje shinikizo limewekwa wazi kwa Rwanda, sasa M23 ndio inajitokeza na kuteseka wakisema, “Sikiliza mimi ndiye mwenye makosa, naondoka Uvira”? Ni dhahiri huu ni ujanja wa kumvuruga mpatanishi ambaye ni Marekani, aliyejitolea kuchukua hatua, kwa sababu ni wazi kuwa kilichotokea Uvira hakikubaliki.”
Hata hivyo, mapigano yanaendelea kusini mwa mji wa Uvira katika eneo la Makobola na milima ya Swima na Kasekezi katika tarafa ya Fizi, kati ya jeshi la Kongo, FARDC, wakishirikiana na Wazalendo dhidi ya waasi wa M23 wanaotaka kusonga mbele kuelekea mji wa Baraka.
Hali hiyo inazusha hofu katika jamii na kusababisha maelfu ya familia kukimbia makwao jambo ambalo Waziri Muyaya amekiri na kusikitikia. “Leo, tuna takwimu ya wakimbizi 200,000. Hali ni tete. Ni wazi, tutafanya sehemu yetu, kuhakikisha kwamba tunatoa makazi, na kuhakikisha wenzetu wanatunzwa vyema popote walipo. Kuna ujumbe umeenda Burundi na mwingine utawasili Tanzania kutathmini mahitaji na rasilimali zote. Lakini nadhani hapa, panahitajika uhamasishaji mkubwa zaidi. Ni lazima kuwe na amani kwani kitu bora tunachoweza kutoa kwa familia zilizohamishwa ni fursa ya kurudi nyumbani.”
Wakati hayo yanajiri muungano wa AFC/M23 unaoungwa mkono na Rwanda, umetangaza mipango ya kupanua shughuli zake zaidi mashariki mwa Kongo.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka wa pili wa vuguvugu hilo, mratibu Corneille Nangaa amesema waasi hao wananuia kuongeza shughuli zao katika jimbo la Ituri, kaskazini mashariki na Katanga kusini mashariki.
Nangaa alilishutumu jeshi la Kongo na washirika wake Wazalendo kwa kuendeleza vurugu katika maeneo ya Masisi, Walikale, Fizi, Minembwe, na Mikenge.
Kundi la M23 liliiteka Uvira mapema mwezi huu bila upinzani kabla ya kutangaza kujiondoa kwa upande mmoja, jambo ambalo lilielezwa kama hatua ya kujenga imani katika kuunga mkono mchakato wa amani wa Doha. Lakini Kinshasa inasisitiza kuwa hatua hiyo ipo kwenye karatasi pekee.
