
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma, imetupilia mbali shauri la maombi ya kibali cha kupinga uamuzi wa kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 2025, lililofunguliwa na wakili Peter Madeleka.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Juliana Masabo, leo, Jumatano, Desemba 17, 2025, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la awali lililoibuliwa na Serikali, ikiomba shauri hilo lifutwe bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.
Katika uamuzi huo, Jaji Masabo amekubaliana na hoja kwamba shauri hilo ni batili kisheria kwa kukiuka kifungu cha 19 cha Sheria ya Maboresho ya Sheria (Kuhusu ajali mbaya na masharti mbalimbali) na kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Masuala ya Rais; Marejeo ya Mwaka 2023.
Hata hivyo, Wakili Madeleka amekata rufaa Mahakama ya Rufani muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali shauri hilo, akiwasilisha mahakamani taarifa ya kusudio lake la kupinga uamuzi huo.
“Ifahamike mrufani katika shauri hilo kutokana na kutokuridhika na uamuzi wa mheshimiwa J. Masabo (Juliana) uliotolewa Dodoma, Desemba 17, 2025. Anakusudia kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi wote,” inasomeka taarifa ya notisi ya rufaa aliyoiwasilisha Mahakama ya Rufani na wakili Madeleka.
Wakili Madeleka alifungua shauri hilo dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kutokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kufuta sherehe za maadhimisho ya Uhuru, Desemba 9, 2025.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Novemba 24, 2025, akisema Rais Samia ameelekeza fedha ambazo zingetumika kwenye sherehe hizo zitumike kukarabati miundombinu iliyoharibiwa wakati wa ghasia za maandamano ya uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025.
Katika hati ya maombi ya shauri hilo alilolifungua Novemba 26, 2025, Wakili Madeleka alikuwa akiomba ruhusa ya mahakama hiyo kufungua shauri la kupinga uamuzi huo kwa utaratibu wa mapitio ya mahakama, kuomba amri tatu.
Amri hizo ni mahakama kufuta uamuzi huo wa Rais, anaouita kuwa si halali na usio na maana, amri ya kumlazimisha kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na amri ya zuio dhidi yake.
Katika kiapo chake na hati ya maelezo yake zilizounga mkono maombi hayo, Wakili Madeleka alidai kuwa uamuzi huo wa Rais kufuta sherehe hizo alioutoa kupitia kwa Waziri Mkuu Novemba 24, 2025, uliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari, likiwemo gazeti la Mwananchi la Novemba 25, 2025.
“Sherehe hizo zilizoelezwa hapo juu huadhimishwa kihalali kila mwaka Desemba 9 na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuenzi Uhuru wa Tanganyika wa Desemba 9, 1961, chini ya uratibu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Madeleka alieleza kuwa yeye ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkazi wa Dar es Salaam, ambaye ana haki ya kusherehekea sherehe hizo chini ya uratibu wa Serikali kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, alidai endapo sherehe za maadhimisho ya siku hiyo za mwaka 2025 hazitafanyika, haki zake zitaguswa kwa kadiri sherehe hizo zinavyomhusu, kwani yeye ni mnufaika halali wa sherehe hizo.
Kwa msingi huo, Madeleka alisema kuwa ndio maana anaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Rais kufuta sherehe hizo, ili aombe mahakama itoe amri tatu dhidi ya uamuzi huo.
Wakili Madeleka alidai kuwa anakusudia kuomba amri hizo, kutengua uamuzi wa Rais ili kuheshimu sheria zilizowekwa za kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika wa Desemba 9, 1961.
Alieleza kuwa Sheria ya Siku za Mapumziko ya Umma [Sura ya 35, Toleo la 2023] inaelekeza kuwa Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 1961, utaadhimishwa kila mwaka Desemba 9.
Hivyo alieleza kuwa ataomba amri ya mahakama kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza sheria zilizoanzishwa za kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika Desemba 9.
Pia alieleza ataomba amri ya kumzuia Rais kuendelea kutekeleza tangazo lake la kusitisha sherehe za kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika za Desemba 9, 2025, kwani kusitishwa kwa sherehe hizo hakujafuata utaratibu; ni kinyume na Katiba na sheria nyingine za nchi.
“Mjibu maombi wa kwanza (Rais) hawezi kuruhusiwa kutumia mamlaka ambayo hana kisheria au ambayo yanakiuka sheria za nchi,” alisisitiza Wakili Madeleka.
Hata hivyo, Desemba 5, 2025, wajibu maombi waliwasilisha kiapo kinzani kujibu maombi hayo sambamba na taarifa ya pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo, wakibainisha sababu mbili za pingamizi hilo dhidi ya shauri hilo.
Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, wajibu maombi waliondoa sababu nyingine ya pingamizi na kubakiza sababu moja, ambayo ndiyo mahakama imekubaliana nayo.
Sababu hiyo ni shauri hilo kukiuka kifungu cha 19 cha Sheria ya Maboresho ya Sheria (Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mbalimbali) na kifungu cha 8(1) cha Sheria ya Masuala ya Rais; Marejeo ya Mwaka 2023.
Jaji Masabo, kwa kuzingatia sababu hiyo, amesema mashtaka yanayomhusu Rais anayepaswa kushtakwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwamba Rais hakupaswa kuunganishwa katika shauri hilo.
Amesema kwa kuangalia kiapo, taarifa za msingi zinamhusu Rais, hivyo akiondolewa katika shauri hilo taarifa zinazobaki ambazo zinamhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali hazitoshelezi kulifanya shauri hilo kusimamiwa mahakamani, kwani linakosa miguu ya kusimamia.
“Kwa sababu hizo, pingamizi linakubaliwa na shauri hili linatupiliwa mbali,” amesema Jaji Masabo.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Madeleka amesema si sahihi, akisema hoja kwamba hakuna ushahidi unaomhusu Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kiapo hilo si pingamizi la kisheria, bali ni suala la ushahidi ambalo halipaswi kujadiliwa katika hatua ya pingamizi, na kwamba kutokana na sababu hizo ndio maana amekata rufaa Mahakama ya Rufani.