Chanzo cha picha, Reuters
-
- Author, Rachel Hagan
Rais wa Marekani Donald Trump ameweka marufuku ya usafiri dhidi ya raia wa Tanzania katika vikwazo vya hivi karibuni vya usafiri.
Ikulu ya White House imesema vikwazo hivyo vinavyokusudia “kulinda usalama wa Marekani” vitaanza kutekelezwa Januari 1, 2026.
Katika amri ya rais ililotiwa saini Jumanne tarehe 16 Disemba, utawala wa Trump uliijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi zinazokabiliwa na vikwazo vya muda vya kuingia Marekani, akitaja uzembe wa ukaguzi, uhakiki na upashanaji habari wa mamlaka ya Tanzania kuhusu raia wao.
Nchi nyingine za Afrika zinazokabiliwa na vikwazo hivyo ni Burkina Faso, Mali, Niger, Sudan Kusini, Syria pamoja na watu walio na pasipoti ya Mamlaka ya Palestina.
Laos na Sierra Leone, ambazo hapo awali ziliwekewa vikwazo vya muda, sasa zimejumuishwa kwenye orodha ya nchi 15 zilizopigwa marufuku, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Tanzania na Zimbabwe.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba Serikali ya Tanzania ilithibitisha kuwa imeanza mashauriano rasmi na Serikali ya Marekani kuhusu masuala ya uhamiaji ambayo ilihofia inaweza kuathiri uwezo wa raia wake kuingia nchini humo.
“Tayari Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya mambo ya nje imeanza kufanya mashauriano na wenzetu wa upande wa Marekani kujua maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa maboresho hususani yanayohusu na masuala ya kikonselu ili kuharakisha Tanzania isiwe moja ya nchi ambazo raia wake watazuiwa kuingia Marekani, alisema Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Mashauriano hayo ya masuala ya kibalozi pamoja na mambo mengine yanagusa utoaji wa nyaraka halali za utambulisho na kushirikiana katika masuala ya uhamiaji.
Kwanini Marekani imechukua hatua hii?
Utawala wa Trump umesema kuwa umechukua hatua hiyo kutokana na kile ilichokitaja kuwa viwango vya juu vya visa vya watu ambao wanasalia nchini muda mrefu baada ya muda wao kuisha kwa jambo la msingi.
Marekani inataka Tanzania na nchi zingine zilizotajwa kurekebisha masuala haya vinginevyo raia wake watapigwa marufuku kuingia Marekani.
Sababu nyingine zilizotajwa na Marekani ni pamoja na nchi zilizoathiriwa kutoa uraia kwa wawekezaji bila masharti ya kuishi nchini humo, pamoja na madai ya matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi na Marekani yanayofanywa na raia wa mataifa hayo wakiwa Marekani.
Hatua hii ya hivi punde ikianza kutekelezwa itawaathiri raia wa nchi husika kuanzia wafanyabiashara, wanafunzi na wengine wanaokwenda kwa shughuli mbalimbali.
Tangazo hilo lilifuatia baada ya kukamatwa kwa raia wa Afghanistan anayeshukiwa kuwapiga risasi askari wawili wa ulinzi wa kitaifa mwishoni mwa wiki, na kuifanya Ikulu ya White House ilielekeza katika kuangazia wasiwasi wake wa usalama.
Chanzo cha picha, EPA
Hii ni mara ya tatu kwa Trump kuweka marufuku ya kusafiri.
Wakati wa muhula wake wa kwanza, alianzisha agizo kama hilo mnamo 2017, ambalo lilizua maandamano na changamoto za kisheria ndani na nje ya nchi. Sera hiyo baadaye ilizingatiwa na Mahakama ya Juu ya Marekani.
Ikulu ya White House ilisema vikwazo vitaendelea kuudmishwa hadi nchi zilizoathirika zifanye “maboresho ya kuaminika” katika usimamizi wa vitambulisho, upashanaji habari na ushirikiano na mamlaka ya uhamiaji ya Marekani.
Vigezo kadhaa vinatumika na marufuku hiyo haitaathiri wakaazi halali wa kudumu, wengi walio na viza, wanadiplomasia au wanariadha wanaosafiri kwa hafla kuu za michezo. Maafisa walisema msamaha wa kesi kwa kesi pia utapatikana ambapo kusafiri kunachukuliwa kuwa kwa masilahi ya kitaifa.
Katika muhula wake wa kwanza wa urais, Rais Trump aliweka marufuku ya safari dhidi ya mataifa yaliyo na idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu, hatua ambayo ilizua mjadala mkali na hata kupingwa mahakamani kabla ya Mahakama ya Juu kuiruhusi katika toleo lake la tatu mwaka 2018.
Marufuku hiyo ilifutwa na Rais Joe Biden, lakini Trump ambaye amekuwa akishughulikia kwa ukubwa wake masuala ya uhamiaji, ameahidi kuirejesha tena akiwa madarakani kwa awamu ya pili, akisema, “itakuwa kubwa zaidi ya mwanzo”.
Mataifa yaliyowekewa marufuku:
- Afghanistan
- Burkina Faso
- Burma
- Chad
- Equatorial Guinea
- Eritrea
- Haiti
- Iran
- Laos
- Libya
- Mali
- Niger
- Jamhuri ya Congo
- Sierra Leone
- Somalia
- Sudan Kusini
- Sudan
- Syria
- Yemen
- Watu walio na vitambulisho vilivyotolewa na Mamlaka ya Palestina au hati za usafiri zilizoidhinishwa pia zimewekewa marufuku ya kuingia Marekani
Vikwazo vya muda:
- Angola
- Antigua and Barbuda
- Benin
- Burundi
- Côte d’Ivoire
- Cuba
- Dominica
- Gabon
- The Gambia
- Malawi
- Mauritania
- Nigeria
- Senegal
- Tanzania
- Togo
- Tonga
- Venezuela
- Zambia
- Zimbabwe
Kesi maalum:
- Turkmenistan (Vikwazo kwa wahamiaji bado vinatekelezwa lakini vimeondolewa kwa wale walio na viza ambazo sio za wahamiaji)
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi