Polisi nchini Australia wamefungua mashtaka mazito dhidi ya mshukiwa wa shambulio la kigaidi lililotokea Jumapili katika ufukwe wa Bondi, mjini Sydney, ambapo watu 15 waliuawa katika shambulio hilo lililowalenga Wayahudi waliokuwa wakisherehekea sikukuu ya Hanukkah.
Mshukiwa huyo, Naveed Akram, mwenye umri wa miaka 24, ameshtakiwa kwa makosa 59, yakiwemo mashtaka 15 ya mauaji, kosa moja la utekelezaji wa kitendo cha kigaidi, pamoja na makosa 40 ya kujaribu kuua watu walioumia. Polisi pia wamesema alihusika katika kuweka vilipuzi karibu na jengo kwa nia ya kusababisha madhara.
Akram ameshtakiwa Jumatano baada ya kuamka kutoka katika hali ya kutokuwa na fahamu akiwa amelazwa hospitalini chini ya ulinzi mkali wa polisi. Baba yake, Sajid Akram, mwenye umri wa miaka 50, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa majibizano kwenye eneo la tukio.
Mashtaka mazito na maswali ya usalama
Kamishna wa polisi wa New South Wales, Mal Lanyon amesema polisi wanasubiri hali ya kiafya ya mshukiwa iwe imetengemaa ili kuhakikisha anaelewa kikamilifu kinachoendelea, jambo linalohitajika kwa misingi ya haki na sheria.
”Kwa sasa tunasubiri hali yake ya kiafya iwe katika kiwango kinachofaa ili tuweze kufanya hilo. Ni muhimu ahakikishe ana uwezo wa kutosha wa kiakili wakati huo. Unapokuwa unatumia dawa, kwa kuzingatia haki yake, ni lazima tuhimize na kuhakikisha kuwa anaweza kuelewa kikamilifu kinachoendelea.”
Kwa mujibu wa polisi, washambuliaji hao wawili walifyatua risasi katika hafla ya Hanukkah iliyokuwa imekusanya familia nyingi, wakiwemo watoto. Zaidi ya watu 20 bado wanapatiwa matibabu hospitalini. Waathirika wote waliotambuliwa hadi sasa ni Wayahudi, kuanzia mtoto wa miaka 10 hadi manusura wa mauaji ya Wayahudi, Holocaust mwenye umri wa miaka 87.
Mazishi ya waathirika yafanyika
Wakati huo huo, mamia ya waombolezaji wameanza kuizika miili ya waathiriwa huku ulinzi mkali wa polisi ukiimarishwa karibu na masinagogi na maeneo ya mazishi. Mazishi ya kwanza yalikuwa ya Rabbi Eli Schlanger, mwenye umri wa miaka 41, baba wa watoto watano na mmoja wa waandaaji wa sherehe hiyo ya Hanukkah.
Mamlaka ya Australia imesema shambulio hilo linaaminika kuhamasishwa na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislami, IS. Uchunguzi unaendelea kubaini iwapo washukiwa walikutana na makundi yenye misimamo mikali wakati wa safari yao nchini Ufilipino mwezi Novemba.
Waziri Mkuu wa Jimbo la New South Wales, Chris Minns amesema kipaumbele cha serikali ni kuhakikisha wahusika wanakabiliwa na sheria na kwamba haki inapatikana kwa waathiriwa na familia zao.
”Hili ni jambo muhimu sana; kwa sasa, kipaumbele cha polisi ni kuhakikisha mashtaka yanafanikiwa na haki inapatikana kwa waathiriwa, na hakuna chochote kinachopaswa kuzuia hilo,” alisema waziri mkuu Minns.
Shambulio hilo limeibua mjadala mkubwa kitaifa kuhusu usalama wa jamii za Wayahudi, ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi, pamoja na udhibiti wa silaha. Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, ameahidi kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya chuki na pia kuimarisha sheria za umiliki wa bunduki.
Wakati taifa likiendelea kuomboleza, Waustralia wengi wamejitokeza kuonyesha mshikamano kwa kutoa damu, kushiriki ibada za kumbukumbu, na kuahidi kuwa hofu haitashinda umoja wa kijamii.
Chanzo: RTRE,AFPE,APE,DPAE