
Dar es Salaam. Mwaka 2025 uko karibu kufikia ukingoni. Unaweza kuwa miongoni mwa miaka iliyobeba mitihani zaidi katika mawanda ya kisiasa nchini.
Ndani ya mwaka huo, kumeshuhudiwa mtikisiko mkubwa wa kisiasa, athari katika mshikamano wa Taifa, mambo yaliyoibua hoja ya haja ya upatanishi wa kitaifa.
Lakini, mwaka huo huo kwa upande mwingine, umekuwa na fursa kiuchumi, marekebisho ya sera za ndani na nje na kuimarisha juhudi za kidiplomasia.
Hata hivyo, fursa hizo zimefunikwa na changamoto za kisiasa zilizozua mjadala kuhusu uwiano kati ya maendeleo, haki na amani.
Ilianza na Chadema
Mitihani katika mwaka 2025 ilianza na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya kuingia katika uchaguzi wake wa ndani uliomwangusha aliyekuwa mwenyekiti wake kwa zaidi ya miongo miwili, Freeman Mbowe.
Umekuwa mtihani kwa sababu vuguvugu la kampeni za nafasi ya uenyekiti iliyowashindanisha Mbowe na Tundu Lissu, kuhusisha maneno yaliyowagawa wafuasi wao na kuzaa mpasuko wa ndani ya chama.
Hilo likawa ufunguo wa kuzaliwa kwa timu Mbowe na timu Lissu hata kabla ya uchaguzi. Baada ya matokeo, Lissu akaibuka kidedea, huku chama hicho kikibaki na majeraha ya misuguano ya kabla ya uchaguzi.
Timu Mbowe na Lissu ziliendelea hata baada ya uchaguzi kuisha, mamia ya wanachama walikihama chama hicho kufuatana na kushindwa kwa Mbowe. Ikawa furaha kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kilichowavuna wanachama hao.
Kati ya mamia waliokihama chama hicho, walikuwamo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Chama, John Mrema na Makada wengine wengi.
Hatua hiyo ilikitikisa chama hicho na kutishia nguvu ya upinzani nchini.
Maofisa wa Serikali walivyogeuka wakosoaji
Ndani ya mwaka 2025 ndipo waliokuwa watumishi waadilifu wa Serikali katika nafasi za kidiplomasia, Balozi Humphrey Polepole na Dk Willibrod Slaa walipogeuka kuwa wakosoaji wakubwa wa mamlaka.
Ukiacha uungwaji mkono walioupata kutoka kwa baadhi ya wananchi, serikalini waliambulia zawadi ya kuvuliwa hadhi ya ubalozi na hatimaye kurejea kuwa raia wa kawaida.
Polepole aliiwakilisha Tanzania katika nchi za Malawi na baadaye Cuba, huku Dk Slaa aliiwakilisha nchi katika mataifa ya Nordic.
Hatua hiyo ilitafsiriwa kama mabadiliko makubwa ya kisiasa kutoka ndani ya mfumo wa dola.
ACT – Wazalendo na kigingi cha urais
Wakati Chadema ikiendelea kusafiri katika barabara yenye milima na mabonde makali, Chama cha ACT – Wazalendo, kilijikuta kikikosa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano, Oktoba 29.
Hili lilianza kwa chama hicho kumpokea mwanasiasa mwandamizi aliyeachana na Chama chake cha Mapinduzi (CCM), Luhaga , ambaye alitumikia nafasi ya ubunge katika Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu kwa miaka 20 na akiitumikia pia Serikali katika mafasi mbalimbali ikiwamo ya uwaziri.
Kupokelewa kwa Mpina ndani ya Chama cha ACT – Wazalendo, ilikuwa shangwe kwa makada wa chama hicho, lakini hatua yake ya kupitishwa kuipeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais, ndiyo iliyozua mitihani.
Mmoja wa makada na viongozi wa chama hicho, aliibuka na pingamizi la uteuzi wake. Likafika kwa uongozi wa chama, mara kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, hatimaye kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na akaondolewa katika kinyang’anyiro cha kiti cha urais katika uchaguzi mkuu huo.
Mambo hayakuwa madogo, ACT – Wazalendo na Mpina wao wakaenda mahakamani, wakashinda na akarudishwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani na akarudisha fomu ya uteuzi.
Mara pah! Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari akapinga uteuzi wake. Isivyo bahati, Mpina akaondolewa tena kwenye kinyang’anyiro hicho cha urais.
Akajaribu tena mahakamani, akakwaa kisiki na uchaguzi ulifanyika bila yeye kugombea.
Hiyo ikaufanya mwaka 2025, kuwa pekee kwa uchaguzi kufanyika bila wagombea urais wa vyama viwili vikuu vya upinzani.
Yaani Chadema ambacho hakikushiriki na ACT – Wazalendo ambacho mgombea wake alienguliwa.
Licha ya kuibuka kwa mijadala kuwa uchaguzi huo usingekuwa na ushindani bila wagombea kutoka vyama hivyo, zilikuwa mithiri ya kelele za chura, hazikuwa kikwazo kwa tembo kunywa maji.
Kampeni zilizokosa mvuto, ushindi wa kihistoria
Hakuna ambaye alikuwa hafahamu kwamba mwaka 2025 mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa kuwachagua madiwani, wabunge na Rais. Kilipofika sasa kipindi cha kampeni, hazikushuhudiwa kashikashi kama ilivyo kawaida. Ni kama zilidorora.
Kukosekana kwa wagombea wenye mizania sawa ya ushindani, ndiyo sababu iliyotajwa kuchochea anguko hilo la kampeni kama ilivyowahi kuelezwa na Profesa Mohamed Makame, mchambuzi wa masuala ya siasa, alipozungumza na Mwananchi.
“Mabadiliko ya watu na mifumo ya siasa ni jambo la kawaida katika siasa, kwani hali inabadilika na vivyo hivyo jamii nayo inabadilika.
“Kubadilika kwa mbinu za wagombea kutoka siasa za mikutano kwenda kampeni za nyumba kwa nyumba ni ishara kuwa wagombea wanataka kuwafikia watu na kuongea nao kwa karibu zaidi,” anasema.
Katika hoja yake hiyo, anasema kampeni hizo ziliegemea upande mmoja, CCM ilijikuta ikishiriki uchaguzi na wapinzani wasio na ushindani hali iliyopunguza mjadala wa sera kampeni za baadhi ya wagombea kutawaliwa na ahadi zisizotekelezeka.
Lakini, historia nyingine ikaandikwa kwa mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan kushinda kwa asilimia 97.66 ya kura, ushindi ambao haujawahi kutokea tangu uhuru wa Tanganyika.
Ushindi huo, licha ya kuonesha uimara wa CCM, uliibua maswali kuhusu afya ya demokrasia ya vyama vingi.
Mlima wa Uchaguzi Mkuu 2025
Mwaka 2025, ukawa na dosari za kisiasa na kiusalama ndani yake. Siku ya uchaguzi kulizaliwa maandamano yaliyozaa vurugu na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.
Vuguvugu la maandamano hayo, lilianzia kwenye changamoto za kisheria zilizolalamikiwa na vyama vya upinzani, wengi wakisema hazikutoa mizania sawa ya ushindani kati ya chama tawala na wapinzani.
Lakini, Serikali ilibaki na msimamo wake kuwa ilishafanya marekebisho madogo ya sheria za uchaguzi na kuweka baadhi ya vipengele kikiwamo cha kuondoa suala la mgombea kupita bila kupingwa na Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi.
Kwa maneno mafupi baadhi ya wanasiasa walidai kwamba kulikosekana maridhiano. Uchaguzi ukafanyika katika hali ya kila upande kukubali kutokubaliana hivyo mioyoni mwa wapinzani kukabaki madukuduku na baadhi ya wanaharakati wakaamua kuratibu maandamano kupitia mitandao ya kijamii.
Kutokubaliana huko ndiko kulikoifanya Chadema isishiriki uchaguzi huo kwa kuanzisha kampeni ya ‘No Reforms No Election.’ Kweli bwana hakikushiriki.
Tarehe ya uchaguzi ikapangwa na ukafanyika na matokeo ndiyo kama nilivyoeleza hapo juu.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusisitiza kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika chaguzi, hivyo kushuka kwa hamasa ya wananchi kuliongeza mlima wa kisiasa kuelekea uchaguzi huo.
“Demokrasia siyo kitu cha kuonekana tu, lazima iwe ya kweli kwa wananchi wote, bila ubaguzi,” Moja ya kauli za Mwalimu Nyerere aliposisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mchakato wa uchaguzi.
Kauli hiyo aliyotoa mwaka 1962 jijini Dar es Salaam, imeendelea kubeba uzito mkubwa, hasa katika muktadha wa milima ya kisiasa iliyojitokeza nchini mwaka 2025, mshikamano wa Taifa umeonekana kutikiswa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu.
Maandamano yaliyozaa vurugu na giza la kitaifa
Katika hatua iliyoishangaza Dunia, siku ya uchaguzi Jumatano, Oktoba 29, 2025 yaliibuka maandamano yaliyozua vurugu kutoka kwa vijana wengi waliokuwa wakipinga mchakato wa uchaguzi na masuala mengine.
Maandamano hayo yalizuka katika maeneo mbalimbali yakitikisa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mara na Mbeya na katika maeneo kadhaa ukiwemo mji wa Kahama, Tarime na Tunduma.
Aidha, baadaye maandamano hayo yaligeuka kuwa vurugu, yakisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, tukio lililoonyesha kwa uwazi kiwango cha hasira na kukata tamaa miongoni mwa vijana, kundi linalohisi kutengwa katika mchakato wa kisiasa.
Kufuatia hatua hiyo, Taifa linamaliza mwaka 2025, likiwa njia panda ya kihistoria yenye milima na mabonde ya kisiasa.
Tangu kufanyika kwa uchaguzi huo uliogubikwa na vurugu, licha ya kauli mbalimbali na juhudi za serikali na wadau mbalimbali, changamoto kadhaa zimeendelea kujitokeza zikiwamo shinikizo na maagizo kutoka Taasisi za Kimataifa kuhusu mustakabali wa siasa za Tanzania.
Rais Samia ameendelea kusimama imara, serikali ikikabiliana na changamoto zote za ndani na nje katika kuhakikisha Taifa linabaki pamoja na kuendeleza juhudi za maendeleo.
“Tanzania haitadhibitiwa au kuamriwa na watu wa nje jinsi ya kuendesha masuala yake ya kisiasa au kiutawala. Tunaheshimu maoni ya wadau wa nje, lakini hatutakubali maagizo au shinikizo.
“Hatuwezi kuruhusu watu au makundi yanayotumia taarifa zisizo sahihi, ndani au nje ya nchi, kutugawanya Watanzania na kuvuruga mshikamano wetu wa kitaifa,” amekuwa akisisitiza mara kwa mara Rais Samia tangu ulipoibuka mzozo huo wa kisiasa kufuatia uchaguzi mkuu nchini.
Hatua za kujitegemea kiuchumi, kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii yanayolenga kuchochea migogoro na kusisitiza uandishi wa habari wa kimkakati unaolinda maslahi ya nchi, ni miongoni mwa hatua zinazosisitizwa na wadau wa amani na serikali katika kuliepusha Taifa na mipasuko iliyotokea.
Hata hivyo, milima na mabonde hayo yamefungua ukurasa mpya kwa Taifa kutathmini, kujenga upya imani ya wananchi na kuimarisha misingi ya demokrasia ili kulinda mshikamano wa Taifa na mustakabali wa demokrasia ya Tanzania iliyojengwa katika miamba imara tangu nchi ipate uhuru mpaka sasa.