Yumkini tatizo la ukosefu wa usalama kwenye mipaka ya Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda likapatiwa ufumbuzi, baada ya nchi hizo nne za mashariki mwa Afrika kuunda baraza la viongozi, ambalo kwa pamoja litashughulikia na kusuluhisha mizozo ya mara kwa mara katika eneo hilo la mipaka, ambako wanaishi watu wa jamii ya Ateker waliotenganishwa na mipaka iliyochorwa na wakoloni.
Eneo hilo limekabiliwa na migogoro ya muda mrefu, inayotokana kwa sehemu kubwa na wizi wa mifugo usiojali mipaka ya mataifa.
Baraza hilo la viongozi kutoka mataifa hayo manne ambayo lilitangazwa rasmi katika kikao kilichofanyika mjini Lodwar, Kenya mwanzoni mwa Desemba 2025, likitwishwa jukumu la kuzungumza na wananchi wao ili kukomesha visa vya wizi mipakani na kusaidia katika juhudi za upatanishi.
”Tunahitaji kuboresha uhusiano kama jamii za wafugaji wakati huu ambapo kuna tatizo la mabadiliko ya tabianchi. Hatuwezi kusalia wafugaji milele, kwa hivyo ni sharti tuwe na mbinu nyingine ya kujikimu,” alisema Beatrice Askul, Waziri wa Kenya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na maeneo kame, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo.
Watu wamoja waliotenganishwa na mipaka bandia
Jamii ya Ateker inaenea kutoka kaskazini mashariki mwa Uganda, kaskazini magharibi mwa Kenya, kusini mashariki mwa Sudan Kusini hadi kusini magharibi mwa Ethiopia. Inaundwa na makabila yenye lugha moja lakini yenye lahaja tofauti, huku wakiwa na mila zinazofanana.
Makundi muhimu katika jamii hiyo ni Wakaramajong na Iteso wa Uganda, Waturkana wa Kenya, Watoposa wa Sudan Kusini na Nyangatom wa Ethiopia.
Waziri Beatrice Askul alisema ”ukweli kwamba watu wa jamii zote hizo wanasikilizana kwa lugha bila kuhitaji mkalimani ni kigezo muhimu cha kurahisisha maridhiano, na kuwezesha utunzaji wa amani mipakani.”
Viongozi wanaounda baraza hilo jipya walikutana kwa siku tatu, na walimaliza kwa kuweka azma ya kupata mwafaka kuhusu uhusiano kwenye mipaka ya mataifa hayo manne ambayo kwa muda mrefu, wakazi wake wamekuwa katika malumbano kutokana na kugombania rasilimali katika shuguli zao za ufugaji.
Msururu wa visa vya uhalifu ulioacha vifo, majeraha na machungu
Mnamo miaka ya hivi karibuni mizozo ya kuvuka mipaka ilitokana na wizi wa ng’ombe, misuguano ya kugombania rasilimali za malisho na maji, ikirahisishwa na mipaka inayoonekana kwenye ramani, lakini haiko bayana ardhini.
Wafugaji 32 wa Kiturkana kutoka Kenya walikamatwa nchini Uganda Aprili 2023, walipokwenda kuiba ng’ombe katika vijiji vya mpakani vya Urum na Lokiriama. Wimbi la uhalifu wa aina hiyo liliendelea hadi mwaka 2024, likihusisha wizi wa kutumia silaha za moto na ubakaji.
Marais wa Kenya na Uganda, William Ruto na Yoweri Museveni, walikubaliana Julai 2025 kuweka mkataba wa matumizi ya pamoja ya rasilimali za maeneo ya mpaka baina ya nchi zao, lengo mojawapo likiwa ni kumaliza mizozo ya miongo mingi na kuwawezesha wenyeji kuishi kwa amani.
”Makubaliano haya juu ya matumizi ya rasilimali baina ya jamii za Karamajong na Turkana, yatakuza maelewano baina ya jamii zote zinazoishi mpakani,” alisema Rais Ruto wakati huo.
Kutimia kwa ndoto ya muda mrefu
Kulingana na Peter Lokeris, mbunge anayesimamia masuala ya Karamoja nchini Uganda, azma ya kuwa na chombo cha ushirikiano miongoni mwa jamii zilizogawanywa kwa mpaka za Ateker imekuwepo kwa muda mrefu, na alielezea furaha kuwa hatimaye imetekelezwa.
”Tumekuwa tukitamani kuwa na baraza kama hili tangu miaka ya 1970 ila imewezekana wakati huu. Ni vizuri kuwa na amani kwa sababu ni kupitia hali ya utulivu ndipo maendeleo hufikiwa,” alisema mbunge huyo.
Aidha, baraza hilo la viongozi kwa kauli moja limekubaliana kubadilisha mitazamo ya wakazi wake kuhusu uwiano na utangamano na kuboresha maisha yao.
Mjumbe Maalum wa Amani katika Ukanda wa Ateker John Munyes, alisema kwamba baraza hilo pia litajadili mbinu za kutumia rasilimali zilizopo kuwanufaisha wakazi akitaja mifano ya kuwepo kwa madini kama dhahabu na mafuta, akisema zinaweza kuchangia ustawi wa maeneo hayo iwapo amani na usalama vitadumishwa.
Wazee wa kimila wakosowa kutengwa katika mchakato huo
Wazee kutoka jamii ya Turkana ambao kijadi ndio wenye dhamana ya uongozi, wamewakosoa waandaaji wa mkutano uliounda baraza hilo kwa kutowashirikisha katika mchakato wa kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakumba watu wao.
Mwenyekiti wa baraza la wazee kutoka eneo la Turkana mashariki, Ekale Eyaran ameiambia DW kuwa licha ya mchango wa watu wa rika lake kwenye masuala ya amani mpakani, waratibu wa mkutano huo uliofanyika Lodwar waliwapuuza.
”Sisi tumekasirika kabisa. Ingestahili tuandae tambiko la kuhalalisha baraza lililoundwa, lakini hatukupata mwaliko. Hivi karibuni tutatangaza msimamo wetu kuhusu baraza hilo,” alionya mzee Eyaran.
Miongoni mwa wajumbe maalum waliohudhuria hafla hiyo ni katibu katika wizara ya maeneo kame wa Kenya Kello Harsama,- Afisa katika wizara ya masuala ya kigeni wa Ethiopia Fitsum Girma, na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayesimamai miundombinu, Andrea Ariik Malueth.
