
Kwa uchache raia 104 wameuawa katika mashambulizi ya droni, ndege zisizo na rubani katika eneo la Kordofan nchini Sudan tangu Desemba 4 mwaka huu. Hayo yametangazwa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk na kuelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka vita na mapigano kati ya makundi ya RSF na SAF huko Sudan.
“Katika tukio moja, shambulio la ndege zisizo na rubani lilipiga skuli ya chekechea na hospitali moja huko Kalogi, Kordofan Kusini. Shambulio hilo liliua raia wasiopungua 89, wakiwemo wanawake wanane na watoto 43,” amesema Volker Turk.
Vilevile amelaani mauaji ya maafisa sita wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa huko Kadugli, Kordofan Kusini, siku ya Jumamosi, akionya kwamba mashambulizi dhidi ya maafisa wa kulinda amani yanaweza kuhesabiwa kuwa ni jinai za kivita.
Siku ya Jumapili, shambulio tofauti la ndege zisizo na rubani kwenye hospitali huko Dilling, Kordofan Kusini, liliua watu wasiopungua sita na kujeruhi wengine 12, wakiwemo wafanyakazi wa masuala ya matibabu, amesema Turk, akibainisha kuwa vituo vya matibabu na wafanyakazi vinalindwa na sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu.
Eneo la Kordofan, ambalo linajumuisha majimbo ya Kaskazini, Magharibi na Kordofan Kusini, limekumbwa na mapigano makali katika wiki za hivi karibuni kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), na kupelekea makumi ya maelfu ya watu kukosa makazi. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Sudan imekumbwa na mapigano baina ya majenerali wa kijeshi tangu Aprili 15, 2023 ambayo yameshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.