Tunduma/Dar. Kiini cha msongamano wa magari unaoukabili mpaka wa Tunduma mkoani Songwe ni zaidi ya wembamba wa barabara. Yapo mengi yanayohusishwa na hali hiyo, vikiwemo vitendo vya rushwa.

Sambamba na rushwa, wamiliki binafsi wa maegesho ya magari wameingia lawamani, wakitajwa kushiriki mchezo wa kusababisha msongamano huo ili kutengeneza mazingira ya kujiingizia kipato.

Wakati hali ikielezwa hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema zipo athari za kiuchumi zinazosababishwa na msongamano huo, hasa kuifanya Tanzania ionekane kikwazo badala ya kichocheo cha biashara ya kikanda.

Wanakwenda mbali zaidi na kueleza msongamano huo utawalazimu wafanyabiashara kutafuta njia mbadala za usafirishaji, jambo linaloweza kupunguza matumizi ya bandari, hivyo kupunguza fursa za uwekezaji na fedha za kigeni.

Msongamano huo wa malori ya mizigo una athari za kiuchumi, na haziishii mpakani hapo pekee bali huzigusa sekta nyingi za uchumi wa taifa na kikanda.

Msongamano si wa leo wala jana

Msongamano wa malori katika eneo hilo haukuanza leo wala jana, ni tukio linalojitokeza kila wakati, na zimewahi kutajwa mbinu mbalimbali za kupata suluhu bila mafanikio.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, Aprili 2025, aliunda kamati ya uchunguzi wa chanzo cha msongamano huo, lakini suluhu haikupatikana.

Hata wakati Chongolo, ambaye sasa ni Waziri wa Kilimo, akiunda kamati hiyo, tayari zilishafanywa juhudi mbalimbali na viongozi waliopita, ikiwemo kujenga vituo vya mizani, lakini bado msongamano uliendelea.

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, Julai 2022, aliagiza kujengwa barabara ya njia nne kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma ili kukomesha msongamano huo.

Juhudi zote hizo zinatokana na ukweli kwamba msongamano katika eneo hilo umekuwa mithiri ya donda ndugu. Zipo nyakati malori yanatumia hadi siku nane kusubiri kuvuka kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Tatizo mawakala

Wapo wanaohusisha msongamano huo wa malori na mchezo mchafu unaochezwa na mawakala wa magari, wakishirikiana na wamiliki wa maegesho ili wapate chochote kitu, kama inavyoelezwa na Shaibu Mohamed, mmoja wa madereva.

Kwa mujibu wa Mohamed, mawakala hao hutengeneza mazingira ya kuchelewesha nyaraka za kuruhusu magari kuvuka mpakani ili mengi yalazimike kulipa tozo ya maegesho, ambayo mawakala hupata mgawo.

Katika ufafanuzi wake, anasema katika Sh5,000 ya ada ya maegesho inayotozwa gari moja, wakala hupata mgawo wa Sh2,000 na mmiliki wa maegesho hubaki na Sh3,000.

“Mawakala huchelewesha nyaraka makusudi ili gari inapoegeshwa zaidi kwenye maegesho yao, wapate kiasi hicho cha Sh2,000 kwa kila Sh5,000 ya gari lililoegeshwa,” anasema Mohamed.

Lawama nyingine iliyowaangukia mawakala inatolewa na Katibu wa Taasisi ya Madereva Tanzania, Nelson Mpinzile, aliyesema dereva wa gari analazimika kutoa kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 ili kuruhusiwa kuvuka haraka.

“Nakupatia majina ya kampuni za mawakala wanaojifanya miungu watu kwa kusababisha foleni, hivyo bila kudhibiti utendaji wao, hata ijengwe barabara ya njia sita au nane, foleni itaendelea kuwepo,” anasema.

Ucheleweshwaji nyaraka

Sababu nyingine iliyotajwa na madereva ni ucheleweshaji wa nyaraka za magari ya mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hasa yale yanayobeba mizigo ya kawaida, huku yale ya matenki yakipata nyaraka kwa wakati, kama anavyoeleza dereva Hassan Yusuph.

Kwa mtazamo wake, kuna haja na umuhimu wa mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mamlaka nyingine kusomana ili kutoa huduma kwa uwiano na kwa haraka.

Polisi lawamani

Msongamano huo wa magari umeliingiza Jeshi la Polisi katika lawama, kwa maelezo ya Yusuph, aliyesema baadhi ya askari huwalazimisha madereva kuingiza magari katika maegesho ya Chimbuya.

Anataka uchunguzi ufanyike kubaini sababu ya askari hao kuwalazimisha madereva kuegesha katika maegesho hayo yanayomilikiwa na mtu binafsi.

Mawakala wajibu tuhuma

Katibu wa Mawakala wa Kituo cha Forodha Tunduma, Masudi Mandimo, anakana tuhuma za mawakala kushirikiana na wamiliki wa maegesho, akisema utendaji wao unazingatia miongozo.

Anasema mawakala hawahusiki kusababisha msongamano huo, bali wanashirikiana na Jeshi la Polisi kuvusha magari, kwa kuwa kazi yao ni kutafuta wateja na kuwawakilisha mabosi wao waliopo Dar es Salaam, pamoja na kutengeneza nyaraka za magari yanayotoka Zambia na Kongo kwenda Dar es Salaam.

RC aonya rushwa

Akizungumza baada ya hoja za pande mbili, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame, anawaonya watendaji mpakani hapo kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwataka kutoa huduma kwa misingi na ubora unaotakiwa.

Katika kikao chake na vyama vya madereva, madereva na taasisi za Serikali, anawaelekeza viongozi wa madereva wa malori wafanyekazi bila kuchochea migogoro, bali wawasaidie madereva kutatua changamoto zinazowakumba wanapokuwa kazini.

“Serikali imeanza kutafuta fedha za dharura kwa ajili ya kutatua changamoto ya foleni ndani ya miezi minne katika mpaka wa Tunduma, ikiwemo kujenga barabara ya njia nne kutoka Kilimanjiro kuelekea upande wa Zambia. Hili ni agizo la Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kwa Tanroads alipofanya ziara hivi karibuni mpakani hapo,” anasema.

Barabara kutanuliwa

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alifanya ziara katika eneo hilo Desemba 12, 2025, na kuiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kufanya tathmini ya kutanua barabara katika mpaka wa Tunduma mkoani Songwe.

Alitaka zitafutwe fedha za haraka na za dharura, ifanyike tathmini na kupanua ili kuwezesha ujenzi wa barabara ya tatu.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza Wakala wa Barabara (Tanroads), ameagiza kufanya tathmini ya kutanua barabara katika mpaka wa Tunduma.

Ulega ametoa agizo hilo akiwa Tunduma mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia wasafirishaji na wananchi wa eneo hilo kutokana na msongamano wa malori.

Alisisitiza wizara hiyo imejipanga kujenga mzani mwingine katika eneo la Iboya ili kuruhusu magari yote yanayotoka Tunduma kwenda Mbeya kupima uzito na kupunguza msongamano.

Aliwataka mameneja wa Tanroads wa mikoa ya Mbeya na Songwe kuhakikisha wanaimarisha barabara za mchepuo zitakazopunguza foleni ya magari katika ukanda huo.

Athari kiuchumi

Msongamano wa malori ya mizigo katika mpaka wa Tunduma una athari za kiuchumi, na haziishii mpakani hapo pekee bali huzigusa sekta nyingi za uchumi wa taifa na kikanda, kama inavyoelezwa na mchambuzi wa uchumi, Profesa Benedict Mongula.

Anasema malori yanapokaa hadi siku nane bila kuvuka, gharama za uendeshaji huongezeka kutokana na matumizi ya mafuta, posho za madereva, matengenezo ya magari na ada mbalimbali.

“Gharama hizi hulipwa na wafanyabiashara na, hatimaye, hubebwa na mtumiaji wa mwisho kupitia kupanda kwa bei za bidhaa, hivyo kuchochea mfumuko wa bei na kupunguza uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha,” anasema.

Athari nyingine, anasema ni kupungua kwa ufanisi wa minyororo ya ugavi, jambo linalosababisha ucheleweshaji wa bidhaa muhimu kama chakula, dawa, pembejeo za kilimo na malighafi za viwandani.

Anaeleza viwanda vinapokosa malighafi kwa wakati hulazimika kupunguza uzalishaji au kusimamisha shughuli, hali inayopunguza mapato ya Serikali kupitia kodi na kuathiri ajira.

“Kwa nchi inayojipambanua kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari, msongamano wa muda mrefu Tunduma unadhoofisha hadhi hiyo na kuibua mashaka kwa wafanyabiashara wa kikanda,” anasema Profesa Mongula.

Anasema kuchelewa kwa malori pia kunasababisha upotevu wa bidhaa zinazoharibika haraka, hususan mazao ya chakula, mboga, matunda na bidhaa za mifugo.

Hasara hizo, anasema huwagusa moja kwa moja wakulima, wasafirishaji na wafanyabiashara wadogo ambao tayari wana mitaji midogo.

Upotevu huo, anasisitiza, unapunguza mapato ya kaya, unavunja mzunguko wa fedha katika maeneo ya uzalishaji na, hatimaye, kudhoofisha uchumi wa ndani, hasa katika mikoa inayotegemea biashara ya kuvuka mipaka.

Kwa upande wa mapato ya taifa, Profesa Mongula anasema msongamano huathiri ukusanyaji wa kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na biashara ya mipakani.

Malori yanapokwama kwa muda mrefu, anaongeza, kasi ya mzunguko wa biashara hupungua, idadi ya safari inapungua na hivyo kupunguza kiwango cha mapato kinachoweza kukusanywa kwa kipindi husika.

Pia anasema msongamano huo unaifanya Tanzania ionekane kama kikwazo badala ya kichocheo cha biashara ya kikanda, kwani wafanyabiashara wataanza kutafuta njia mbadala za usafirishaji, jambo linaloweza kupunguza matumizi ya bandari na kuathiri uwekezaji, mapato na fedha za kigeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *