Serikali ya Tanzania imewataka Watanzania wote wanaosafiri kwenda Marekani kuzingatia kikamilifu masharti ya viza zao, kufuatia uamuzi wa Marekani kuiweka Tanzania kwenye orodha ya nchi zenye vikwazo visivyokamilika (partial restrictions) vya kuingia nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, uamuzi huo umetokana na idadi kubwa ya Watanzania kukaa Marekani kwa muda mrefu zaidi ya ulioidhinishwa kisheria, hususan kwa visa za biashara na utalii pamoja na visa za wanafunzi na mafunzo ya ufundi na programu za kubadilishana.

Taarifa za Marekani zinaonyesha kiwango cha Watanzania wanaokaa kinyume cha masharti ya viza kimefikia asilimia 8.3 na asilimia 13.97 zaidi ya kiwango kinachokubalika kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ya Tanzania imeanza mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani kupitia Wizara za Mambo ya Nje za pande zote mbili, kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa haraka na wa kudumu ili kuondolewa kwa vikwazo hivi.

“Wakati jitihada hizo zikiendelea, Serikali inasisitiza Watanzania kuheshimu masharti ya viza zao na kuondoka Marekani mara muda wa viza unapokamilika, ili kuepuka madhara zaidi kwa hadhi ya nchi na kusaidia kurekebisha hali hii,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, nchi nyingine zilizowekwa katika utaratibu huu ni Angola, Benin, Côte d’Ivoire, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe.

✍ @claud_jm
#AzamTVUpdates

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *